Biryani ya nyama ya kusaga (kofta)

Muda wa maadalizi; dakika 45
Muda wa kupika; lisaa 1 dakika 15
Muda jumla; Masaa 2

Mahitaji

Kwa wali

Vikombe 2 mchele wa basmati
½ kijiko cha chai jira
Punje 3 za iliki
Vikombe 4 maji ya moto
Chumvi kwa kuonja

Kwa nyama/ Kofta

500g/ nusu kg nyama ya kusaga
Kitunguu maji 1 kikubwa (kitunguu #1)
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu
Kijiko 1 cha chakula tangawizi
Kijiko 1 cha chakula garam masala
Vijiko 1½ vya chakula tomato sauce
¼ kikombe majani ya giligilani
Chumvi kwa kuonja

Kwa kutengeneza sosi/ gravy

Nyanya 2 kubwa
Kitunguu maji 1 kikubwa (kitunguu #2)
Kijiko 1 cha chai tangawizi
Kijiko 1 cha chai kitunguu saumu
Kijiko 1 cha chakula garam masala
Punje 3 karafuu
Kijiko 1 cha chai unga wa giligilani
¾ kijiko cha chai binzari ya pilau
½ kijiko cha chai manjano
Kipande cha mdalasini
¾ kikombe maji ya moto
Vijiko 5 vya chakula mafuta ya kupikia

Viungo vya juu/ garnish

Kitunguu maji 1 cha wastani (kitunguu #3)
Zafarani kiasi
Vijiko 3 vya chakula maziwa ya uvuguvugu
Vijiko 3 hadi 4 vya chakula majani ya giligilani

Maelekezo

Hatua ya 1; Maandalizi

Andaa mchele kwa kuuosha hadi maji yawe masafi kabisa. Loweka kwenye maji kwa muda wa dakika 30. Ukiloana, chuja maji weka pembeni

Andaa viungo vya nyama; katakata kitunguu #1 vipande vya mraba vidogovidogo, katakata majani ya giligilani. Twanga kitunguu saumu na tangawizi, weka pembeni

Andaa viungo vya sosi/ gravy; katakata nyanya na kitunguu #2 vipande vidogovidogo vya mraba; twanga tangawizi na kitunguu saumu, weka pembeni

Andaa viungo kwa ajili ya juu/ garnish; Katakata kitunguu maji #3 vipande virefu; katakata na majani ya giligilani

Loweka zafarani chache kwenye vijiko 3 vya chakula maziwa ya uvuguvugu. Weka pembeni

Hatua ya 2; maandalizi ya nyama na wali

Katika bakuli kubwa, changanya viungo vyote ya nyama; nyama ya kusaga, kitunguu #1 kilichokatwakatwa vipande vidogovidogo vya mraba, ¼ kikombe majani ya giligilani, kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu, kijiko 1 cha chakula tangawizi, Vijiko 1½ tomato sauce, Kijiko 1 cha chakula garam masala na chumvi kwa kuonja

Gawanya nyama kwenye vipande kama 12 hadi 15, tengeneza umbo la mduara au mpira mdogo. Hifadhi kwenye sahani, weka pembeni

Kwenye sufuria katika moto wa juu kiasi, chemsha vikombe 4 vya maji. Ongeza mchele, jira, iliki na chumvi. Pika mpaka wali ukaribie kuiva. Ipua, chuja maji. Weka pembeni

Hatua ya 3; Kupika

Kwenye sufuria katika moto wa wastani, chemsha mafuta. Ongeza kitunguu #3 ulichokatakata vipande virefu kwenye mafuta. Kaanga mpaka kitunguu kiwe na rangi ya kahawia ila kisiungue

Toa kitunguu kwenye mafuta, hamishia kwenye sahani iliyotandazwa tissues za jikoni au chujio la bati ili mafuta yachuje. Weka pembeni kwa ajili ya kuweka juu ya biryani badae

Kwenye mafuta yaleyale baada ya kutoa kitunguu, ongeza kitunguu #2 kilichoandaliwa kwa ajili ya sosi. Kaanga mpaka kilainike

Ongeza kijiko 1 cha chai tangawizi na kijiko 1 cha chai kitunguu saumu, vivivyoandaliwa kwa ajili ya sosi. Acha viive hadi vilainike, kwa dakika kama 2

Ongeza viungo vikavu vilivyoandaliwa kwa ajili ya sosi; giligilani ya unga,  binzari ya pilau, pilipili ya unga, garam masala na manjano. Acha viive kwa dakika 2 hadi 3

Ongeza nyanya zilizokatwakatwa

Kaanga mpaka nyanya ziive vizuri na zilainike kabisa

Ongeza ¾ kikombe cha maji ya moto. Ongeza na chumvi kwa kuonja

Ongeza nyama kwenye mchanganyiko. Weka taratibu zisambaratike. Acha nyama ziive bila kugeuzwa kwa dakika kama 4

Geuza taratibu upande wa pili, acha ziive kwa dakika 4 nyingine

Pika mpaka nyama iive vizuri na sosi iwe nzito, ibakie kama kikombe 1

Hatua ya 4; kupangilia biryani

Katika sufuria nyingine kubwa zaidi iliyopakwa mafuta kwa chini, sambaza nusu ya wali chini ya sufuria. Sambaza nyama na sosi yake juu ya wali

Sambaza wali uliobakia juu ya nyama; ongeza na majani ya giligilani yaliyakatwakatwa kwa ajili ya kuweka juu pamoja na kitunguu cha kukaanga. Nyunyizia kwa juu maziwa yenye zafarani. Funika sufuria, acha wali uive kwa moto wa chini kabisa kwa dakika 20 hadi 30; au mpaka wali uive vizuri. (unaweza pia kupalilia kwa mkaa, au kuoka kwenye oven katika chombo chenye mfuniko)

Changanya vizuri

Tenga cha moto

Unaweza kula na kachumbari ya mtindi, tango na majani ya mnanaa au ya tango na mtindi

Enjoy

Leave a Reply