Meat pie za samli; zimeongezwa na mbogamboga

Maandalizi; dakika 40
Muda wa kupika; dakika 30
Muda jumla; lisaa 1 dakika 10

Mahitaji

Kupata uhakika na kutumia viungo sahihi, endapo jina la kiungo limewekewa mstari, bofya kwenye mstari kuona picha ya kiungo

Kwa kukandia unga


Vikombe 2 unga wa ngano
½ kikombe mafuta ya samli
Kijiko 1 cha chai baking powder
½ kikombe pamoja na vijiko 3 vya chakula buttermilk (maji au maziwa)
¼ kijiko cha chai chumvi
Yai 1 kwa ajili ya kupaka juu

Mahitaji ya nyama

500g/ nusu kilo nyama ya kusaga
Karoti 2 za wastani
Hoho nusu x3 (kijani, njano na nyekundu)
Kitunguu maji 1 kikubwa
Vijiko 2 vya chakula kitunguu saumu
Kijiko 1 cha chakula tangawizi
½ kikombe majani ya kotmiri na mnanaa
Vijiko 2 vya chakula mafuta ya kupikia (yakihitajika)
Chumvi kwa kuonja

Maelekezo

Kwenye bakuli kubwa, changanya unga wa ngano, chumvi, baking powder na mafuta ya samli. Changanya vizuri kwa mkono mpaka uwe kama chenga chenga

Ongeza ½ kikombe cha buttermilk (maji au maziwa) uanze kukanda, endelea kuongeza kijiko kimoja kimoja cha  buttermilk (maji au maziwa) mpaka unga ushikane vizuri. Kanda hadi ulainike kabisa

Funika bakuli na kitambaa kisafi cha jikoni, acha unga utulie kwa dakika kama 10-20

Wakati unga unatulia, anza kutengeneza nyama za kujaza sambusa. Katakata kitunguu, karoti na hoho vipande vya mraba vidogovidogo sana. Twanga kitunguu saumu na tangawizi; katakata majani ya kotimiri na mnanaa vipande vidogovidogo sana. Weka pembeni

Kwenye kikaangio katika moto wa wastani, weka nyama, tangawizi na kitunguu saumu. Weka chumvi na pilipili manga kwenye nyama. Endapo nyama ni kavu ongeza vijiko 2 vya chakula vya mafuta, kama ina mafuta usiweka mafuta. Pika mpaka nyama iive vizuri, huku ukigeuza geuza, kama dakika 15

Ongeza kitunguu maji na karoti. Pika kwa dakika nyingine 2 hadi 3, huku ukigeuzageuza

Ongeza hoho upike kwa dakika nyingine 2

Ipua sufuria kwenye jiko. Changanya na majani ya kotimiri na mnanaa, weka pembeni

Washa oven joto la 170 degrees C, au andaa jiko la mkaa kwa ajili ya kuoka. Wakati jiko linapata moto, kanda unga tena, ugawanye kweye madonge madogomadogo ya mduara 20. Weka madonge ya unga kwenye sehemu iliyonyunyiziwa unga, acha yapumzike kwa dakika chache

Sukuma kila donge utengeneze umbo la mduara kama la chapati; litakuwa dogo kulinganisha na chapati na isiwe nyembamba sana

Weka kijiko na nusu hadi vijiko viwili vya nyama katikati ya mduara uliosukuma. Usijaze sana, ukijaza sana itakuwa ngumu kufunga. Hakikisha unabakiza nafasi ya kufungia

Inua upande mmoja huku ukishakikisha nyama inabakia katikati, funika ncha zikutane upande wa pili

Tumia uma kufunga ncha za meat pie, funga vizuri isibakia na matobo

Rudia mpaka umalize zote. Panga meat pie kwenye chombo cha kuokea kilichopakwa mafuta au karatasi za kuokea. Piga yai, paka yai lililopigwa juu ya meat pie kwa kutumia brush au kijiko

Oka kwenye oven iliyopata moto kwa dakika 20 hadi 25 minutes; au mpaka zipate rangi ya kahawia kwa mbali na ziive vizuri

Pakua kama utakavyopenda

Enjoy

 

4 Replies to “Meat pie za samli; zimeongezwa na mbogamboga”

Leave a Reply