Biryani ya nyama ya kuku

Maandalizi; dakika 45
Muda wa kumarinate; masaa 4+
Muda wa kupika; lisaa 1 dakika 15
Muda jumla; Masaa 2 + muda wa kumarinate

Mahitaji

Kupata uhakika na kutumia viungo sahihi, endapo jina la kiungo limewekewa mstari, bofya viungo vyenye mstari kuona picha ya kiungo. Kupata picha na majina ya viungo mbalimbali bofya hapa

Kwa wali

Vikombe 2 mchele wa basmati
½ kijiko cha chai mbegu za jira (cumin seeds)
Star anise 1
¾ kijiko cha chai chumvi

Kwa nyama

Kilo 1 nyama ya kuku
Kijiko 1 cha chakula tangawizi
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu
Kijiko 1 cha chakula chicken bouillon powder
½ limao
¼ kikombe mafuta ya mzaituni (olive oil)

Kwa kutengeneza sosi/ gravy

Vijiko 2 vya chai tangawizi
Vijiko 2 vya chai kitunguu saumu
Kitunguu maji 1 kikubwa
Vijiko 3 vya chakula mafuta ya samli/ mafuta ya kupikia
Pilipili kichaa 2
Nyanya 3 kubwa
½ kilo viazi ulaya
½ kikombe mtindi
½ kijiko cha chai pilipili ya kukausha (chili pepper flakes)
Vijiko 2 vya chai garam masala
Kipande cha mdalasini
Bay leaf 2
Punje 4 karafuu
Punje 4 iliki
½ kijiko cha chai mbegu za jira
Kijiko 1 cha chai unga wa giligilani
Kijiko 1 cha chai binzari ya manjano
Chumvi kwa kuonja

Viungo vya juu/ garnish

Kitunguu maji 1 cha wastani
Zafarani kiasi
¼ kikombe maji ya uvuguvugu
¼ kikombe majani ya giligilani
¼ kikombe majani ya mnanaa
Mafuta ya kukaangia kitunguu

Maelekezo

Hatua ya kwanza; Kumarinate nyama

Toa ngozi na kuchanja nyama; Andaa viungo vya kuku; twanga kitunguu saumu na tangawizi; kamua maji limao

Kwenye bakuli kubwa, changanya vizuri kuku na viungo vyote vya kuku

Funika bakuli au weka nyama kwenye mfuko. Acha viungo vikolee kwa masaa 4 au inapendeza zaidi akikaa  usiku kucha

Hatua ya pili; maandalizi

Ukiwa tayari kupika, andaa mchele kwa kuuosha hadi maji yawe masafi kabisa. Loweka kwenye maji kwa muda wa dakika 30

Ukiloana, chuja maji weka pembeni

Andaa viungo vya sosi/ gravy; katakata pilipili vipande vidogovidogo vya mraba; katakata viazi ukubwa utakaopenda; twanga kitunguu saumu na tangawizi, weka pembeni

Weka nyanya na kitunguu maji kwa ajili ya sosi kwenye mashine ya kusagia chakula kutengeneza rojo, weka pembeni

Andaa viungo kwa ajili ya juu/ garnish; Katakata kitunguu maji vipande virefu; katakata na majani ya giligilani na majani ya mnanaa, weka pembeni

Loweka zafarani chache kwenye ¼ kikombe cha maji ya uvuguvugu. Weka pembeni

Hatua ya tatu; Kupika

Washa oven katika joto la 150 degrees C. Kwenye sufuria katika moto wa juu kiasi, chemsha vikombe 4 vya maji. Ongeza mchele, mbegu za jira, star anise na chumvi. Pika mpaka wali ukaribie kuiva

Ipua, chuja maji. Weka pembeni

Kwenye kikaangio katika moto wa wastani kaanga kitunguu kwa ajili ya kuweka juu (garnish) mpaka kiwe na rangi ya kahawia ila kisiungue

Toa kitunguu kwenye mafuta, hamishia vitunguu kwenye sahani iliyotandazwa tissues za jikoni au chujio la bati ili mafuta yachuje. Weka pembeni kwa ajili ya kuweka juu ya biryani badae

Ukitoa kitunguu, weka viazi kwenye mafuta. Kaanga mpaka viive vizuri, ipua weka pembeni

Kwenye sufuria katika moto wa chini kiasi, weka mafuta ya kupikia au samli. Yakichemka ongeza kitunguu saumu, tangawizi na pilipili kichaa. Pika paka viive na harufu ya ubichi iishe, kama dakika 2

Ongeza kuku na viungo vizimavizima; mdalasini, mbegu za jira, karafuu na iliki. Kaanga kwa dakika 5, ukigeuza mara chache isishike chine

Ongeza rojo ya nyanya, majani la bay na viungo vikavu vilivyoandaliwa kwa ajili ya sosi; giligilani ya unga, pilipili ya kukausha, manjano na garam masala. Acha ipike mpaka nyanya ziive vizuri

Ongeza mtindi, koroga vizuri, ongeza na chumvi ikibidi

Funika sufuria, acha nyama iive taratibu kwenye moto wa chini kwa dakika kama 10, ukigeuza inapobidi; au mpaka sosi iwe nzito, ibakie kama kikombe 1 cha kuivisha wali

Hatua ya 4; kupangilia biryani

Ongeza viazi changanya vizuri na sosi. Katika chombo cha kuokea au sufuria nyingine kubwa zaidi sambaza nyama chini ya sufuria

Sambaza wali juu ya nyama. Ongeza na majani ya giligilani, majani ya mnanaa yaliyakatwakatwa kwa ajili ya kuweka juu pamoja na kitunguu cha kukaanga. Nyunyizia kwa juu maji yenye zafarani

Funika na foil, acha wali uive kwenye oven iliyopata moto kwa dakika 20 hadi 30; au mpaka wali uive vizuri. (unaweza pia kupalilia kwa mkaa, au kuoka kwenye oven katika chombo chenye mfuniko)

Changanya vizuri

Tenga cha moto na kachumbari ya tango, nyanya na mtindi; au ya tango na mtindi

Enjoy

31 Replies to “Biryani ya nyama ya kuku”

  1. jamani..simple and delicious..hivi unaweza kupika biryani kilocal?kuna vitu hapo sijui vinapatikana wapi haswa viungo..

Leave a Reply