Makaroni ya nyama ya kusaga

Maandalizi; dakika 5
Muda wa kupika; dakika 25
Muda kwa jumla; dakika 30

Mahitaji

250g/ robo kilo nyama ya kusaga
250g/ robo kilo makaroni
Kitunguu maji kimoja cha wastani
Nyanya 2
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu na tangawizi
Vijiko 3 vya chakula mafuta ya kupikia
Kijiko 1 cha chakula beef seasoning
Kikopo 1 nyanya ya kopo 140g ( au 2 x 70 g)
Pilipili manga kwa kuonja
Chumvi ikihitajika
Jibini ya chaguo lako ya kunyunyizia juu (ukipenda)

Maelekezo

Saga nyanya na kitunguu maji kwenye mashine ya kusagia kupata rojo, weka pembeni

Chemsha makaronii kulinganya na maelekezo ya kwenye pakiti, ipua dakika 2 kabla ya kuiva. Osha na maji ya baridi ili yasishikane, weka pembeni

Kwenye sufuria katika moto wa juu kiasi, chemsha mafuta. Ongeza nyama ya kusaga, beef seasoning, kitunguu saumu na tangawizi pamoja na pilipili manga. Kaanga kwa dakika kama 5, au mpaka nyama ianze kupata rangi ya kahawia

Ongeza rojo ya nyanya na kitunguu. Koroga vizuri, funika na mfuniko. Acha nyama iive moto wa wastani kwa dakika kama 10, au mpaka iive vizuri na maji yakaukie

Ongeza nyanya ya kopo na maji kiasi. Funika tena, pika kwa dakika kama 5; au mpaka sosi iwe nzito ila isikauke

Ongeza makaroni kwenye mchanganyiko wa nyama na maji kidogo yakihitajika. Changanya vizuri. Ongeza na chumvi kiasi ikihitajika

Pakua na jibini kama utapenda

Leave a Reply