Egg Chops za nyama na unga wa mchele

Photo credit; Laissa Miller
Maandalizi; dakika 20
Muda wa kupika; dakika 15
Muda jumla; dakika 35

Mahitaji

Mayai 8 makubwa au 10 madogo
500g/ nusu kilo nyama ya kusaga
Kitunguu 1 cha wastani
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu na tangawizi
Kijiko 1 cha chai bizari ya manjano
½ kijiko cha chai cayenne pepper
Kijiko 1 cha chai garam masala powder
¼ kikombe majani ya kotimiri/ giligilani
Chumvi kwa kuonja
½ kikombe unga wa mchele
Mafuta ya kukaangia

Maelekezo

Kwenye sufuria ya wastani katika moto wa juu kiasi, chemsha mayai yaive kama unavyopenda. Wakati mayai yanachemka, andaa viungo vingine; katakata majani ya kotimiri na kitunguu vipande vodogovidogo sana

Katika bakuli kubwa; weka nyama, kitunguu, majani ya kotimiri, kitunguu saumu na tangawizi, bizari ya manjano, pilipili ya unga na garam masala. Vunja yai moja uongeze kwenye mchanganyiko. Changanya vizuri, weka na chumvi kwa kuonja

Gawanya mchanganyiko kwenye madonge 6 hadi 8 yaliyolingana (inategemea na ukubwa wa mayai). Menya na mayai, weka pembeni

Funika kila yai na donge moja ya nyama. Hakikisha yai linakuwa katikati na limefunikwa vizuri na nyama. Sawazisha vizuri kwa juu kisha paka unga wa mchele kwenye madonge ya nyama kwa juu, hakikisha kila sehemu imefunikwa vizuri

Chemsha mafuta kwenye kikaangio katika moto wa wastani. Wakati mafuta yanachemka, piga yai moja lililobakia. Chovya kila egg chop kwenye yai, tingisha kidogo ili yai lililozidi litoke kabla ya kuweka kwenye mafuta

Kaanga mpaka ziwe na rangi ya kahawia

Hamishia egg chops zilizoiva kwenye sahani iliyowekwa tissues za jikoni au chujio la bati ili mafuta yote yachuje

Pakua kama utakavyopenda

Enjoy

 

22 Replies to “Egg Chops za nyama na unga wa mchele”

  1. Sijutii kukufollow mpnz. Naomba kuuliza hzo nyama za kusaga huichemshi hata kidogo. Na hilo yai bichi unachanganya kwenye nyama ee. Me nlikua najuaga hilo donge la nje ni mkate uliokandwa unachanganywa na nyama ya kusaga au samaki.

    1. kwa recipe hii huitaji mkate, ni nyama mbichi isiyochemshwa, ukiichemsha itasambaratika haitashikana, itaiva kwenye kukaanga. Na yai bichi unachanganya kwenye nyama ili ishikane vizuri, unachanganya na viungo vingine kama maelekezo

Leave a Reply