Rosti ya meatballs (kababu za nyama)

Maandalizi; dakika 20
Muda wa kupika; dakika 30
Muda jumla; dakika 50

Mahitaji

Kwa meatballs (kababu za nyama)

500g/ nusu kilo nyama ya kusaga
Slesi 2 za mkate
Yai 1
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu na tangawizi
Pilipili kichaa 2 (zisizowasha)
Kitunguu maji 1 cha wastani
Vijiko 3 vya chakula majani ya kotimiri
Vijiko 3 vya chakula majani ya mnanaa
1/4 kikombe maziwa ya uvuguvugu
1/2 kikombe unga wa ngano
Chumvi na pilipili manga kwa kuonja
Vijiko 4 vya chakula mafuta ya kupikia

Kwa rosti ya nyanya

Nyanya 2 kubwa
Kitunguu 1 cha wastani
Kijiko 1 cha chai kitunguu saumu na tangawizi
Kikopo  1 nyanya (gram 70)
Kipande cha mdalasini
Bay leaves 1-2
Vijiko 2 vya chakula mafuta ya kupikia
Kikombe 1 maji
Chumvi na pilipili manga kwa kuonja
Majani ya kotimiri na jibini ya kunyinyizia kwa juu

Maelekezo

Andaa viungo vya sosi; weka nyanya na kitunguu kwenye mashine ya kusagia kutengeneza rojo; twanga kitunguu saumu na tangawizi; katakata majani ya kotimiri vipande vyembamba; weka pembeni

Toa sehemu za pembeni kavu za mkate, katakata kipande cha katikati vipande vidogovidogo

Andaa viungo vya meatballs (kababu za nyama); twanga kitunguu saumu na tangawizi; katakata pilipili kichaa, kitunguu maji, majani ya kotimiri na majani ya mnanaa vipande vidogovidogo

Loweka mkate na maziwa kwenye bakuli, changanya mpaka ulainike kabisa

Kwenye bakuli kubwa, weka nyama, yai, kitunguu saumu, tangawizi, pilipili kichaa, majani ya kotimiri, majani ya mnanaa, kitunguu maji,mchanganyiko wa maziwa na mkate, chumvi na pilipili manga, changanya vizuri kwa mkono

Gawanga nyama kwenye madonge madogomadogo, chovya kwenye unga wa ngano kila upande mpaka nyama ifunikwe kabisa na unga wa ngano

Kwenye sufuria au kikaangio kikubwa katika moto wa juu kiasi, chemsha vijiko 4 mafuta. Ongeza madonge ya nyama. Kaanga kwa dakika 1 hadi 2, au mpaka iwe ya kahawia kwa nje ila isiive kabisa. Pakua nyama kwenye sahani, weka pembeni

Kwenye sufuria/ kikaangio weka vijiko 2 vya chakula mafuta, yakichemka ongeza mdalasinni, bay leaves, kitunguu saumu na tangawizi pika mpaka kitunguu saumu na tangawizi vilainike. Ongeza nyanya ya kopo na rojo ya nyanya na kitunguu. Pika mpaka nyanya ziive vizuri, ukigeuza inapobidi. Ongeza na chumvi na pilipili manga kwa kuonja

Ongeza kikombe 1 cha maji, acha yachemke mpaka sosi ianze kutokota. Ongeza meatballs (kababu za nyama), funika sufuria, acha iive moto wa chini kabisa kwa dakika kama 20 au mpaka nyama iive vizuri na sosi iwe nzito; ukigeuza sosi mara moja moja…

Ongeza majani ya giligilani, pakua tayari kwa kuliwa

Pakua na chakula utakachopenda, Nyunyizia jibini (cheese) kwa juu wakati wa kupakua

Enjoy

Leave a Reply