Wali wa kukaanga wenye kamba wadogo na mbogamboga

Maandalizi; dakika 10
Muda wa kupika; dakika 20
Muda jumla ; dakika 30

Mahitaji

Vijiko 4 vya chakula mafuta ya kupikia
350g kamba wadogo, menya na safisha
Chumvi na pilipili manga (nyeupe) kwa kuonja
Kitunguu maji 1 cha wastani, katakata vipande vidogovidogo
Karoti 1 kubwa, menya na katakata vipande vidogovidogo
1/2 kikombe njegere 
Vijiko 2 vya chai kitunguu saumu
Mayai 2, yapige
Vikombe 3 vya chakula wali uliopikwa
Vijiko 3 vya chakula sosi ya soya nyepesi (light)
Kijiko 1 cha chakula mafuta ya ufuta
1/4 kikombe majani ya kitunguu

Maelekezo

Kwenye kikaango katika moto wa wastani, chemsha vijiko 2 vya mafuta. Ongeza kamba wadogo (shrimps). Wasambaze kwenye kikaango wasibebane, kama kikaango kidogo pika mara 2. Ongeza chumvi na pilipili manga kwa kuonja. Pika kwa dakika kama nne kwa pande zote, wasiive sana wakakauka. Hamishia kwenye sahani

Ongeza kijiko kingine cha mafuta kwenye kikaango, kisha weka kitunguu maji, kitunguu saumu na karoti. Kaanga mpaka vilainike ila visiive sana. Ongeza njegere. Unaweza kuongeza na maji kidogo sana kusaidia njegere ziive vizuri na pia endapo viungo vitashika kwenye sufuria viachie. Endapo utatumia kikaangio cha ambacho hakishiki chini unaweza pia kuongeza maji kiasi kuwivisha tu njegere

Tumia mwiko kuhamishia viungo vyote upande mmoja wa kikaango, kisha ongeza mafuta yaliyobakia upande ulio wazi. Piga mayai, weka kwenye upande wenye mafuta. Yakoroge haraka sana yasipate mabonge kisha changanya kila kitu pamoja kwa haraka

Ongeza wali na kamba wadogo (shrimps) waliokaangwa awali. Changanya mpaka wali upate tu joto, usipike muda mrefu viungo vikaiva sana. Ongeza sosi ya soya na mafuta ya ufuta. Changanya vizuri, weka vitunguu vya majani. Changanya na ipua haraka vitunguu vya majani visiive sana

Pakua cha moto, enjoy

Leave a Reply