Habari! Karibu sana kwenye ukurasa wa mapishi wa JikonaJane

Jina langu ni Jane Wambura, Mtanzania ninayeishi Berlin, Germany. Mimi na mume  wangu tuna mtoto mmoja wa kike mwenye maka 2 anayeitwa Mila ambaye pia anapenda sana kupika. Mtamuona baadaye tukipika wote

Ninapenda sana kupika na kuoka. Kuanzia nikiwa mtoto mdogo, mama yangu alijitahidi sana kunielekeza mapishi mbalimbali aliyoyajua. Nilipofika miaka 10, nilianza kuoka keki ndogondogo za majirani na badae keki za harusi tofauti za kanisani kwetu, wakati huo tulikuwa tunaishi Dodoma. Nilipata pia usaidizi kutoka kwa wamama tofauti kutoka kanisani na majirani kwa sababu walijua nilipenda sana mapishi

Binafsi sikukuu kama Chrismas, Pasaka na Mwaka Mpya ni muhimu sana kwangu. Misimu ya sikukuu nilipenda na bado ninapenda sana kuoka na kupika vyakula vingi tofauti. Furaha yangu kubwa ni kuona watu wakifurahia kula chakula ninachopika. Katika blog ya JikonaJane kutakuwa na mapishi mengi sana ya kupika na kuoka kwa ajili ya milo rahisi ya kila siku na pia sikukuu tofauti kukusaidia wewe kufurahia na familia yako kama mimi nilivofurahia na ninavyoendelea kufurahia na familia yangu

Karibuni sana