Bhajiya au bagia ni kitafunwa ambacho kwa wengi wetu kinaturudisha kwenye kumbukumbu ya utotoni; shuleni wakati wa mapumziko, kwenye migahawa au vibanda vya vyakula, vitafunwa unavyonunua kwa mama fulani anayejulikana mtaa mzima na kadhalika. Kupika bhajiya ni rahisi kuliko wengi wanavyofikiria. Fuatilia recipe ya JikonaJane utupe mrejesho

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Dakika 40 Idadi ya walaji 4 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Kunde zipo za aina tofauti. Kwa Tanzania tumezoea zile zina rangi ya brown. Kama hutazipata unaweza kutumia kunde za aina nyingine, kwa mfano mimi nimetumia black eyed peas

Loweka kunde kwenye maji ya moto kwa sababu maji ya moto yanafanya zilowane vizuri na kuumuka kwa haraka zaidi

Kusaga kunde inakuwa rahisi zaidi endapo zitalala usiku kucha kwenye maji ili zilainike. Kumbuka pia kutumia mashine yenye nguvu kuepuka kuunguza mashine yako. Mbali ya kusaga na blender, unaweza pia kutwanga kwenye kinu na mchi kama una nguvu za kutosha

Viungo vya ziada unaweza kuweka kutokana na matakwa ya mpishi na walaji. Kwa mfano mimi nimeweka maji ya limao, tangawizi na majani ya giligilani. Unaweza kuongeza pilipili na viungo vingine tofauti utakavyopenda

Baking powder inasaidia bhajiya zichambuke vizuri. Unaweza ukatumia au usitumie, uamuzi wa mpishi

Pumzisha mchanganyiko kama muda unaruhusu. Ukishachanganya kila kitu, funika kwenye bakuli kwa lisaa 1 hadi 2 ili viungo vikolee vizuri kabla ya kukaanga

Kaanga moto wa wastani kwenye mafuta yaliyokwisha chemka kuepuka bhajiya zisibabuke na kuwa mbichi kama moto mkali au zisinyonye mafuta kama moto wa chini sana

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

Vikombe 2 kunde
Vitunguu maji 3 vya wastani
Vijiko 2 vya chakula maji ya limao (ukipenda)
Kijiko 1 cha chai baking powder
Kijiko 1 cha chakula tangawizi
1/2 kikombe majani ya giligilani
Chumvi kwa kuonja
Mafuta ya kukaangia

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Osha na kuloweka kunde kwenye maji ya moto siyo chini ya masaa 8, au usiku mzima

Hatua ya 2

Ukiwa tayari kutengeneza, anza kwa kukatakata vitunguu maji, majani ya giligilani na kutwanga tangawizi. Weka pembeni

Hatua ya 3

Weka kunde na maji ya limao kwenye mashine ya kusagia chakula au blender. Unaweza pia kutumia mashine ya mkono ukipenda au kutwanga kwenye kinu. (hakikisha mashine yako ina nguvu ya kutosha kusaga kunde). Kama mashine yako ni ndogo saga kidogokidogo. Saga mpaka ilainike; endapo itakuwa ngumu kusaga ongeza maji kiasi.

Hatua ya 4

Ongeza kitunguu maji, tangawizi na majani ya giligilani kwenye mchanganyiko, saga kwa sekunde kama 10. Hakikisha vitunguu na majani ya giligilani hayasagiki kabisa. Weka mchanganyiko kwenye bakuli kubwa. Ongeza chumvi na baking powder, changanya vizuri

Hatua ya 5

Kama muda unaruhusu, funika bakuli, acha viungo vikolee kwenye friji kwa lisaa 1 hadi 2

Hatua ya 6

Chemsha mafuta kwenye kikaango katika moto wa wastani. Yakichemka, tumia kijiko cha chakula kuchota mchanganyiko wa kunde kuweka kwenye mafuta. Kaanga mpaka ziive vizuri

Hatua ya 7

Pakua na enjoy

Comments

Join discussion.