Butter Chicken ni mboga pendwa ambayo asili yake ni nchini India. Mboga hii hupikwa na minofu ya kuku ndani ya rosti ya nyanya, viungo mbalimbali na siagi. Mboga hii inaweza kuliwa na chakula cha aina yoyote kwa siku za kawaida au hata siku maalum!!DSC08637-3

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Lisaa 1 Idadi ya walaji 4 Rahisi

Mambo ya kuzingatiaDSC08660

Minofu ya kuku unaweza kutumia ya mapaja ya kuku au nyama ya kifua cha kuku. Minofu inapatikana supermakets karibu zote kubwa

Siagi au butter ni kiungo muhimu katika butter chicken ndiyo maana inaitwa butter chicken. Siagi/ butter pia zinapatikana supermarkets

Kumarinate kuku ni muhimu kama unataka nyama yako ipendeze zaidi. Unaweza kumarinate mpaka masaa 72 kabla ya kupika, ikae tu kwenye friji mpaka ukiwa tayari kupika

Olive oil ndiyo mafuta ninayotumia mimi kwa sababu ni mazuri kiafya. Unaweza kutumia mafuta mengine yoyote unayotumia kila siku badala ya Olive oil

Nyanya ya kopo inasaidia kufanya rosti iwe nzito zaidi. Unaweza kuongeza au kupunguza kutokana na matakwa yako

Cooking cream au cream ya kupikia ni moja ya viungo muhimu sana katika butter chicken, zinapatikana supermarkets karibu zote

Tui la nazi siyo kiungo muhimu kwenye butter chicken. Mimi binafsi ninapenda kuchanganya cream na butter chicken, naona inaongeza radha zaidi. Ukipenda tumia cream peke yake bila tui la nazi

Majani ya kotimiti/ giligilani yanaongeza radha kwenye kuku, ni vizuri zaidi endapo utayatumia

Pilipili inapendeza sana kwenye butter chicken. Inaweza kutumia ya unga au fresh. Mimi sikutumia kwa sababu mtoto wangu pia anakula chakula ninachopika

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji ya nyama

1/2 kilo minofu ya kuku
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu na tangawizi
Kijiko 1 cha chai Olive Oil/ mafuta ya kupikia
Kijiko 1 cha chakula chicken flavor
Kijiko 1 cha chai binzari ya manjano
1/4 kijiko cha chai pilipili manga
1/2 ya limao dogo

Mahitaji ya rosti

Vijiko 2 vya chakula Olive Oil/ mafuta ya kupikia
Kijiko 1 cha chakula siagi
Vitunguu 2 vya wastani
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu na tangawizi
Nyanya 2
Kijiko 1-1/2 cha chakula nyanya ya kopo
Kijiko 1 cha chai binzari ya pilau
Kijiko 1 cha chai coriander powder
Chumvi kwa kuonja
1/2 kikombe cream ya kupikia
1/2 kikombe tui la nazi
Majani ya kotimiri/ giligilani kiasi chako

Maelekezo hatua kwa hatua

DSC08630-1

Hatua ya 1

Anza kwa kumarinate minofu ya kuku. Unaweza kuandaa usiku halafu upike kesho yake mchana au jioni, nyama itapendeza zaidi. Katakata nyama vipande vidogovidogo ukubwa wa tonge moja. Weka nyama, paste ya kitunguu saumu na tangawizi, chicken flavor, binzari ya manjano, pilipili manga, kijiko 1 cha mafuta na maji ya limao kwenye bakuli kubwa au mfuko. Changanya vizuri, weka kwenye friji mpaka masaa 72. Inavyozidi kukaa ndiyo inazidi kupendeza

Hatua ya 2

Ukiwa tayari kupika, toa nyama kwenye friji. Andaa viungo; katakata kitunguu, nyanya na majani ya giligilani, weka pembeni

Hatua ya 3

Weka vijiko 2 vya chakula kwenye kikaango au sufuria katika moto wa wastani, yakichemka ongeza minofu ya kuku. Hakikisha nyama hazijabebana, zimekaa kwa usawa kwenye sufuria/ kikaango. Pika kwa dakika kama 2 au mpaka zianze kupata rangi ya kahawia. Geuza mojamoja ili upande wa chini nao upate rangi ya kahawia. Kumbuka nyama haitakuwi kuiva kabisa, itaivia kwenye sosi baadae. Nyama ikiwa tayari, hamishia kwenye sahani weka pembeni

Hatua ya 4

Ongeza siagi kwenye kikaango hichochicho. Weka kitunguu maji na paste ya kitunguu saumu na tangawizi kwenye kikaango kabla siagi haijayeyuka kabisa na kuungua. Kaanga kwa dakika 2-3, au mpaka harufu ya ubichi iishe kwenye kitunguu saumu na kitunguu maji kilainike

Hatua ya 5

Ongeza nyanya, nyanya ya kopo, binzari ya pilau, coriander powder na chumvi. Changanya vizuri, funika acha nyanya ziive vizuri kabisa. Unaweza kuongeza maji kiasi endapo nyanya zitakaukia kabla ya kuiva na kulainika vizuri

Hatua ya 6

Nyanya zikiiva na kulainika vizuri, ongeza tui la nazi na cream. Changanya vizuri kisha acha ichemke mpaka ianze kutokota

Hatua ya 7

Ongeza nyama uliyoikaanga awali. Changanya vizuri. Funika acha iive kwa dakika kama 5-10 kwenye moto wa chini ili isishike chini na viungo vikolee vizuri. Ikiiva na nyama ikiwa imeiva vizuri sosi pia itaongezeka uzito.

Hatua ya 8

Ongeza majani ya giligilani/ kotimiri kisha ipua. Changanya vizuri majani kwenye sosi. Pakua na chakula utakachopenda

Comments

Join discussion.