Dengu ni moja ya mboga zenye protini nyingi na yenye radha nzuri sana ukizipika vizuri. Dengu zinauzwa bei nzuri inayothibitisha kwamba hauhitaji pesa nyingi kula chakula bora kwa mwili wako

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Dakika 55 Idadi ya walaji 6 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Dengu ni laini na hazihitaji kulowekwa wala kuchemshwa kabla ya kupika. Zinahitaji tu kuoshwa na kupikwa kama maelekezo yanavyoonyesha

Chambua dengu kuhakikisha hazina uchafu au vipande vidogovidogo vya mawe. Osha dengu mara kadhaa kabla ya kuzipika kuhakikisha zipo safi na salama

Kiafya dengu ni nzuri sana kwani zinaongeza virutubisho vingi mwilini na pia zina calories chache. Dengu zinaongeza madini mwilini, zina protini, hazina mafuta na zinasaidia kurahisisha mmeng´enyo wa chakula. Imedhibitishwa kwamba dengu pia ni chakula kizuri kwa afya ya moyo.

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

Kikombe 1 dengu kavu
Kijiko 1 cha chakula mafuta ya kupikia
Kikombe 1 tui la nazi
Nyanya 2-3 za wastani
Kitunguu maji 1 cha wastani
Kijiko 1 cha chakula nyanya ya kopo
½ kijiko cha chai binzari ya pilau
½ kijiko cha chai giligilani ya unga
Chumvi kwa kuonja
¾ kijiko cha chai tangawizi
½ kikombe majani ya giligilani

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Osha na kuchuja dengu, weka pembeni. Katakata kitunguu vipande vidogovidogo vya mraba. Saga nyanya kwenye mashine ya kusagia chakula utengeneze rojo. Endapo hutatumia mashine, katakata vipande vidogovidogo sana. Twanga tangawizi

Hatua ya 2

Kwenye sufuria katika moto wa wastani, weka mafuta. Kaanga kitunguu maji mpaka kilainike, kama dakika 3. Usipike kikakauka sana kikabadilika rangi. Ongeza tangawizi, changanya vizuri kwa sekunde chache

Hatua ya 3

Ongeza rojo ya nyanya, nyanya ya kopo, binzari ya pilau, coriander powder na chumvi. Changanya vizuri. Funika, acha mchanganyiko upike kwa dakika kama 5, au mpaka nyanya ziive vizuri

Hatua ya 4

Ongeza vikombe 2 vya maji na dengu kwenye sufuria, changanya vizuri. Funika sufuria, acha dengu ziive katika moto wa chini kwa dakika 20-30; au mpaka dengu ziive kabisa. Kama maji hayatatosha ongeza

Hatua ya 5

Ongeza tui la nazi, acha tui liive moto wa chini sana kwa dakika 5 hadi 7 zaidi. Weka majani ya giligilani na kuipua

Hatua ya 6

Pakua kama utakavyopenda na wali, chapati, ugali, maandazi, naan bread au chakula chochote utakachopenda wewe

Comments

Join discussion.