Keki ya limao ni keki ambayo inatengenezwa na maji ya limao na maganda ya limao ambayo huipa radha halisia ya limao. Kwa wapenzi wa keki au malimao, hii recipe siyo ya kuikosa

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Saa 1 Dakika 10 Idadi ya walaji 8 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Vipimo ni muhimu sana katika kuoka. Kama unataka matokeo mazuri katika uokaji, fuatilia vipimo kama vilivyo, kamwe usikadirie chochote. Tumia vikombe na vijiko maalum kwa kupimia ili kupata matokea mazuri zaidi

Limao ni kiungo muhimu sana katika hii keki. Chagua limao fresh lenye maganda mengi ili kukurahisishia kukwangua maganda. Ni rahisi ukikwangua maganda kwanza kisha kamua maji baadaye

Maji ya limao fresh yanasaidia kuongeza radha fresh kwenye keki, usitumie maji ya limao ya kununua dukani, jitahidi kutumia fresh

Mayai na Siagi kama unahifadhi kwenye friji, hakikisha umetoa lisaa moja kabla ya kutumia. Siagi ikilainika inachanganyikana vizuri zaidi na mayai pamoja na viungo vingine na vilevile kuongeza keki kuchambuka vizuri zaidi. Mayai pia yanachanganyikana vizuri yakiwa siyo ya baridi. Mayai ya baridi yanasababisha viungo vingine kama siagi kuganda na kufanya keki isichambuke vizuri. Endapo umejisahau kutoa kwenye friji, lainisha siagi kwe kuweka kwenye kibakuli juu ya maji ya moto kwa dakika moja au mbili. Kwa mayai, toa kwenye friji kisha weka kwenye maji ya uvuguvugu (siyo ya moto) kwa dakika kama 15

Baking powder na baking soda zote zinahitajika kwenye uokaji wa hii keki. Baking powder na baking soda ni tofauti na zina matumizi tofauti. Tumia zote ili kupata keki nzuri

Kuoka hakikisha umewasha oven moto wa juu na chini na oven imepata joto kabla ya kuweka kwenye oven. Hakikisha pia oven hujawasha moto mkali sana ili keki iive vizuri ndani na isiungue nje

Icing sugar unaweza kufanya nzito kiasi au nyepesi kutokana na upendeleo wako. Ukipenda nzito punguza maji ya limao, anza na kuweka kijiko 1 cha chai kwanza kisha endelea kuongeza kama itakavyohitajika. Angalia picha chini kuona tofauti kati ya icing sugar nyepesi na nzito

Hifadhi keki kwenye kontena kwa siku hadi tatu nje ya friji au siku 6 kwenye friji. Kwa utamu wake haitamaliza siku 3

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji ya keki

1/2 kikombe siagi
Kikombe 1 sukari
Mayai 3 makubwa
Vijiko 2 vya chakula maganda ya limao
Kijiko 1 cha chakula maji ya limao
Vijiko 2 vya chai vanilla
Vikombe 1 1/2 unga wa ngano
1/4 kijiko cha chai baking powder
1/4 kijiko cha chai baking soda
1/4 kijiko cha chai chumvi
1/3 kikombe sour cream (itoe kwenye friji dakika 15 kabla ya kutumia)

Mahitaji ya icing sugar

1/2 kikombe icing sugar
Kijiko 1 cha chakula maji ya limao (na ya ziada ikihitajika)

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Anza kwa kuwasha oven joto la 165 degrees C ili ipate moto wakati unachanganya keki. Paka siagi chombo cha kuokea keki, weka pembeni. Kwangua maganda ya limao na kukamua maji yake, weka pembeni

Hatua ya 2

Kwenye bakuli la wastani, chekecha unga wa ngano, baking soda, chumvi na baking powder weka pembeni

Hatua ya 3

Kwenye bakuli jingine, saga sukari na siagi mpaka ilainike vizuri

Hatua ya 4

Ongeza mayai; moja baada ya jingine huku unachanganya. Koroga mpaka ilainike vizuri kisha weka maganda ya limao, maji ya limao pamoja na vanilla. Changanya vizuri

Hatua ya 5

Ongeza mchanganyiko wa unga wa ngano kidogo kidogo huku ukichanganya na sour cream. Koroga hadi uchanganyike vizuri

Hatua ya 6

Mimina mchanganyiko wako kwenye chombo cha kuokea ulichopaka mafuta awali. Oka keki kwa dakika 55; au mpaka iive vizuri. Ikiiva, acha ipoe kwenye chombo cha kuokea

Hatua ya 7

Wakati keki inapoa, changanya icing sugar na maji ya limao mpaka ichanganyike vizuri

Hatua ya 8

Mimina mchanganyiko wa icing sugar juu ya keki angali ya uvuguvugu. Acha ipoe kabisa na icing sugar yake kisha katakata kama utakavyopenda

Comments

Join discussion.