Keki ya mdalasini ni keki ambayo ni nadra kuisikia na haijulikani na wengi, lakini mara utakapoijaribu utagundua ni keki nzuri sana na tamu sana. Mimi binafsi naipenda wakati wa baridi ninywe na chai ya moto

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Saa 1 Dakika 15 Idadi ya walaji 8 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Mdalasini ndio kiungo muhimu katika hii keki. Tumia mdalasini wa unga siyo kijiti

Mayai na Siagi kama unahifadhi kwenye friji, hakikisha umetoa lisaa moja kabla ya kutumia. Siagi ikilainika inachanganyikana vizuri zaidi na mayai pamoja na viungo vingine na vilevile kuongeza keki kuchambuka vizuri zaidi. Mayai pia yanachanganyikana vizuri yakiwa siyo ya baridi. Mayai ya baridi yanasababisha viungo vingine kama siagi kuganda na kufanya keki isichambuke vizuri. Mayai yasiyo ya baridi husaidia pia keki kuumuka vizuri zaidi. Endapo umejisahau kutoa kwenye friji, lainisha siagi kwe kuweka kwenye kibakuli juu ya maji ya moto kwa dakika moja au mbili. Kwa mayai, toa kwenye friji kisha weka kwenye maji ya uvuguvugu (siyo ya moto) kwa dakika

Baking powder ndiyo inahitajika kwenye uokaji wa hii keki. Baking powder na baking soda ni tofauti na zina matumizi tofauti. Tumia kwa kufuata maelekezo ili kupata keki nzuri

Kuoka hakikisha umewasha oven moto wa juu na chini na oven imepata joto kabla ya kuweka kwenye oven. Hakikisha pia oven hujawasha moto mkali sana ili keki iive vizuri ndani na isiungue nje

Sosi ya mdalasini inapendezesha keki zaidi na kuifanya isiwe kavu. Tengeneza kwa kufuata maelekezo

Hifadhi keki kwa kufunika na nailoni za kufunikia chakula (plastic wrap) kwa siku mbili nje ya friji au wiki moja kwenye friji. Ikikaa sana funika na nailoni weka kwenye freezer kwa muda wa miezi miwili

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji ya keki

Vikombe 2 unga wa ngano
Kijiko 1 cha chakula baking powder
Kijiko 1 cha chakula mdalasini
3/4 kijiko cha chai chumvi
2/3 kikombe siagi
Vikombe 1-1/3 sukari
Vijiko 1-1/2 vya chai vanilla extract
Mayai 3
2/3 kikombe maziwa

Mahitaji ya sosi ya mdalasini

1/2 kikombe sukari
Vijiko 6 vya chakula siagi
1/3 kikombe maji
Kijiko 1 chai vanilla extract
3/4 kijiko cha chai mdalasini

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Washa oven joto la 175 degrees ipate moto wakati unachanganya keki. Paka siagi chombo cha kuokea keki, weka pembeni. Kwenye bakuli la kubwa, changanya unga wa ngano, mdalasini, chumvi na baking powder weka pembeni

Hatua ya 2

Kwenye bakuli jingine, saga sukari na siagi mpaka ilainike vizuri. Ongeza mayai; moja baada ya jingine huku unachanganya.

Hatua ya 3

Koroga mpaka ilainike vizuri kisha weka vanilla. Changanya vizuri

Hatua ya 4

Ongeza mchanganyiko wa unga wa ngano kidogo kidogo huku ukichanganya na maziwa. Koroga hadi uchanganyike vizuri

Hatua ya 5

Mimina mchanganyiko wako kwenye chombo cha kuokea ulichopaka mafuta awali. Oka keki kwa dakika 45; au mpaka iive vizuri. Ikiiva, acha ipoe kwa dakika kama 5 kabla ya kuiweka kwenye sahani. Hamishia keki kwenye sahani. Toboa toboa na kijiki wakati bado ya moto kiasi

Hatua ya 6

Weka viungo vyote vya sosi ya mdalasini kwenye sufuria; sukari, maji, siagi, mdalasini na vanilla. Koroga mpaka siagi na sukari viyeyuke vizuri

Hatua ya 7

Mwagia sosi ya mdalasini kwa juu

Hatua ya 8

Katakata na tenga kama utakavyopenda

Comments

Join discussion.