Red Velvet ni keki yenye muonekano wa kuvutia kutokana na rangi yake na radha ya kipekee. Icing sugar yake isiyo na sukari sana inaongeza ubora wake haswa kwa watu wasiopenda sana sukari

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Saa 1 Dakika 10 Idadi ya walaji 12 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Vipimo ni muhimu sana katika kuoka. Kama unataka matokeo mazuri katika uokaji, fuatilia vipimo kama vilivyo, kamwe usikadirie chochote. Tumia vikombe na vijiko maalum kwa kupimia ili kupata matokea mazuri zaidi

Mayai na Siagi kama unahifadhi kwenye friji, hakikisha umetoa lisaa moja kabla ya kutumia. Siagi ikilainika inachanganyikana vizuri zaidi na mayai pamoja na viungo vingine na vilevile kuongeza keki kuchambuka vizuri zaidi. Mayai pia yanachanganyikana vizuri yakiwa siyo ya baridi. Mayai ya baridi yanasababisha viungo vingine kama siagi kuganda na kufanya keki isichambuke vizuri. Endapo umejisahau kutoa kwenye friji, lainisha siagi kwe kuweka kwenye kibakuli juu ya maji ya moto kwa dakika moja au mbili. Kwa mayai, toa kwenye friji kisha weka kwenye maji ya uvuguvugu (siyo ya moto) kwa dakika 10 mpaka 15

Buttermilk inaweza kuwa changamoto kupata lakini zinapatikana supermarkets. Endapo utakosa unaweza kutengeneza mwenyewe nyumbani kwa kuchanganya kikombe 1 cha maziwa fresh na kijiko 1 cha chakula cha siki nyeupe (white vinegar). Acha ikae kwa dakika 5 kisha tumia kama kawaida

Rangi sahihi ni muhimu sana kwenye uokaji wa keki ya red velvet. Rangi nzuri kwa mtazamo wangu ni zile za gel. Unaweza pia kuulizia kwenye maduka ya vifaa vya keki wanajua rangi gani ni sahihi kwa red velvet

Baking soda ndio inayotumika kwenye uokaji wa hii keki, siyo baking powder. Baking powder na baking soda ni tofauti na zina matumizi tofauti. Tumia baking soda kama inavyohitajika

Kwenye kuoka, ili kupata keki nzuri hakikisha umewasha oven na imepata joto kabla ya kuoka. Pia hakikisha oven imewasha kwenye setting ya joto la juu na chini

Icing sugar ya kupika kama ilivyo kwenye maelekezo ni nzuri zaidi kwani inachanganywa na uji wa unga wa ngano ambao unasaidia isiwe tamu sana. Icing sugar ya kupika pia ina radha nzuri zaidi na rahisi kutengeneza

Unaweza kuipamba keki kutokana na mahitaji yako. Mara nyingi watu hutumia matunda au unaweza kupamba na vifaa vya kupambia kuweka maua na chochote utakachovutiwa nacho

Hifadhi keki kwenye friji/ jokofu mara baada ya kuipamba kwa lisaa kama moja ili icing sugar ishike vizuri kwenye keki. Endapo utaitumia kwa muda mrefu, acha ikae kwenye friji

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube.

Mahitaji ya keki

½ kikombe siagi
1½ kikombe sukari nyeupe
Mayai 2
Vijiko 2 vya chakula cocoa powder
¾ kijiko cha chai rangi nyekundu ya chakula gel (vijiko 4 rangi ya maji)
Kijiko 1 cha chai chumvi
Kijiko 1 cha chai vanilla extract
Kikombe 1 buttermilk
Vikombe 2½ unga wa ngano (uliochekechwa)
Kijiko 1½ cha chai baking soda
Kijiko 1 cha chakula siki

Icing sugar

Vijiko 5 vya chakula unga wa ngano
Kikombe 1 maziwa
Kikombe 1 sukari nyeupe
Kikombe 1 siagi (butter)
Kijiko 1 cha chai vanilla extract

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Washa oven joto la 175 degrees C. Paka vyombo 2 vya kuokea (au kimoja kikubwa uje ukate keki vipande 2). Weka siagi na sukari kwenye bakuli kubwa, piga mpaka ilainike vizuri

Hatua ya 2

Ongeza yai moja moja, endelea kupiga mpaka ilainike vizuri kabisa

Hatua ya 3

Kwenye bakuli nyingine, changanya buttermilk, cocoa powder, chumvi, rangi ya chakula na vanilla extract. Changanya ichanganyike vizuri

Hatua ya 4

Ongeza mchanganyiko wa buttermilk na unga wa ngano kidogokidogo kwenye mchanganyiko wa awali (siagi, sukari na mayai), mpaka ichanganyike vizuri kabisa

Hatua ya 5

Kwenye bakuli ndogo au bilauli, changanya siki (vinegar) na baking soda. Ongeza kwenye mchanganyiko wa keki. Changanya vizuri kutumia kijiko usitumie mashine, usichanganye sana

Hatua ya 6

Mimina mchanganyiko kwenye chombo/ vyombo vya kuokea. Oka mpaka keki iive vizuri; kama dakika 30 au iive vizuri. Ikiiva, ipua, acha keki ipoe kabisa

Hatua ya 7

Wakati keki inapoa, chemsha maziwa na vijiko 5 vya unga wa ngano katika moto wa chini, ukikoroga mfululizo. Acha uchemke mpaka uwe mzito kabisa. Ipua, acha upoe pembeni

Hatua ya 8

Mchanganyiko ukipoa kabisa; Piga sukari na siagi kwenye bakuli kubwa mpaka ilainike vizuri. Ni muhimu kuchanganya kwa muda mrefu ili ilainike kabisa

Hatua ya 9

Ongeza mchanganyiko wa unga wa ngano na maziwa pamoja na vanilla, endelea kupiga mpaka mchanganyiko uwe mlaini kama icing sugar kabisa

Hatua ya 10

Paka juu ya keki na pamba kama utakavyopenda

Comments

Join discussion.