Keki ya vanilla ni moja ya keki rahisi sana kutengeneza ambayo haihitaji mambo mengi wala viungo vingi. Mbali na kuwa keki ya kawaida, ni kati ya keki zinazopendwa sana na kuokwa kwa wingi ukilinganisha na keki nyingine

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Saa 1 Dakika 10 Idadi ya walaji 12 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Siagi, mayai na maziwa kama unahifadhi kwenye friji, hakikisha umetoa lisaa moja kabla ya kutumia. Siagi ikilainika inachanganyikana vizuri zaidi na mayai pamoja na viungo vingine na kuongeza keki kuchambuka vizuri zaidi. Mayai pia yanachanganyikana vizuri yakiwa siyo ya baridi. Mayai ya baridi yanasababisha viungo vingine kama siagi kuganda na kufanya keki isichambuke vizuri. Endapo umejisahau kutoa kwenye friji, lainisha siagi kwa kuweka kwenye kibakuli juu ya maji ya moto kwa dakika moja au mbili. Kwa mayai, toa kwenye friji kisha weka kwenye maji ya uvuguvugu (siyo ya moto) kwa dakika 10 mpaka 15

Baking powder ndio inayotumika kwenye uokaji wa hii keki, siyo baking soda. Baking powder na baking soda ni tofauti na zina matumizi tofauti. Tumia baking powder kama inavyohitajika

Kwenye kuoka, ili kupata keki nzuri hakikisha umewasha oven na imepata joto kabla ya kuoka. Pia hakikisha oven imewasha kwenye setting ya joto la juu na chini

Unaweza kuipamba keki kutokana na mahitaji yako.

Hifadhi keki kwenye friji/ jokofu mara baada ya kuipamba kwa lisaa kama moja ili icing sugar ishike vizuri kwenye keki. Endapo utaitumia kwa muda mrefu, acha ikae kwenye friji

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube.

Mahitaji ya keki

250g siagi (robo kilo)
250g Sukari (robo kilo)
4 Mayai
500g Unga wa ngano (nusu kilo)
1 Kijiko cha chakula baking powder
10 Vijiko vya chakula maziwa fresh
1 Kijiko cha chakula vanilla
1 Kijiko cha chai chumvi

Icing sugar

¼ kikombe siagi
½ kikombe jibini (cream cheese)
Vikombe 2 icing sugar
Kijiko 1 cha chai vanilla extract
Vijiko 2 vya chakula maziwa, na zaidi ikihitajika

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Washa oven joto la 165 C degree ipate moto wakati unachanganya keki. Paka siagi na unga wa ngano chombo cha kuokea keki, weka pembeni

Hatua ya 2

Kwenye bakuli la wastani, chekecha unga wa ngano, chumvi na baking powder weka pembeni

Hatua ya 3

Kwenye bakuli jingine, changanya sukari na siagi mpaka ilainike kisha ongeza mayai; moja baada ya jingine pamoja na vanilla. Changanya vizuri

Hatua ya 4

Ongeza mchanganyiko wa unga wa ngano kwenye bakuli, koroga hadi uchanganyike vizuri

Hatua ya 5

Malizia kwa kuweka maziwa kidogokidogo huku ukikoroga mpaka unga ulainike kabisa

Hatua ya 6

Mimina mchanganyiko wako kwenye chombo cha kuokea ulichapaka mafuta awali

Hatua ya 7

Oka keki kwa dakika 35 hadi 50 kutegemea na chombo cha kuokea; au mpaka iive vizuri. Ikiiva, acha ipoe kiasi kwenye chombo cha kuokea, kisha ihamishie kwenye waya ya kupozea keki mpaka ipoe kabisa

Hatua ya 8

Wakati keki inapoa, tengeneza icing sugar. Koroga siagi na jibini (cream cheese) kwenye bakuli kubwa mpaka ilainike vizuri

Hatua ya 9

Ongeza icing sugar na vanilla. Endelea kukoroga kwa dakika 1 hadi 2; halafu weka maziwa kidogokidogo mpaka upate uzito unaohitaji

Hatua ya 10

Paka kwenye keki kama utakavyopenda

Comments

Join discussion.