Maharagwe au mboga ya taifa kwa jina la utani ni mboga pendwa yenye virutubisho vingi sana inayoliwa kila siku kwa karibu kila familia. Mbali na kupendwa sana, kuna wakati unaweza kuyachoka. Kuepuka kuyachoka, unaweza kubadilisha jinsi unavyoyapika na viungo unavyotumia
Yaliyomo kwenye ukurasa huu:
Dakika 30 | Idadi ya walaji 4 | Rahisi |
Mambo ya kuzingatia
Maharagwe yachemshwe yaive kabisa kabla ya kuunga kwani kwenye kuunga unatumia muda mfupi sana. Unaweza pia kutumua maharagwe ya aina tofauti kwa recipe hii
Nyanya fresh zinapendeza zikiwa kiasi sana. Usiweke nyingi zikaharibu radha ya maharagwe. Unaweza pia kuongeza nyanya ya kopo kiasi.
Curry powder ni kiungo muhimu kwa recipe hii. Unaweza pia ukaongeza viungo vingine kama coriader powder, garam masala n.k
Kitunguu saumu na tangawizi pia kinafanya curry sauce iwe na radha ya kupendeza zaidi. Unaweza pia kuongeza na kupunguza kutokana na matakwa yako
Tui la nazi nimetumia la kununua siyo ya kukuna nyumbani. Ukiweka tui kwenye maharagwe punguza moto ili isishike chini na kuuguza maharagwe
Maji siyo lazima kuweka. Endapo utaridhika na uzito wa tui la nazi unaweza kutokuweka maji
Maji ya limao yanapendeza zaidi yakiongezwa mwishoni kabisa wakati umeshamaliza kupika na kuipua mboga jikoni
Majani ya giligilani au kotimiri unaweza kutumia kiasi utakachopenda wewe mpishi au walaji
Video
Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube
Mahitaji
1/2 kilo maharagwe yaliyochemshwa
Vijiko 2 vya chakula mafuta ya kupikia
Kitunguu maji 1 kikubwa
Nyanya 1 kubwa
Kijiko 1 cha chakula curry powder
Chumvi kwa kuonja
Pilipili manga kwa kuonja
Kikombe 1 tui la nazi
1/2 maji limao (kijiko 1 cha chakula au kiasi chako)
Majani ya kotimiri/ giligilani
Maelekezo hatua kwa hatua
Hatua ya 1
Anza kwa kuandaa viungo. Katakata kitunguu maji na nyanya vipande vidogovidogo vya mraba. Katakata na majani ya giligilani/ kotimiri, weka pembeni
Hatua ya 2
Ukiwa tayari kupika, chemsha mafuta kwenye kikaango au sufuria. Ongeza kitunguu maji pamoja na paste ya kitunguu saumu na tangawizi. Kaanga mpaka kilainike kiwe na rangi ya kahawia kwa mbali, na harufu ya ubichi ya kitunguu saumu iishe
Hatua ya 3
Ongeza nyanya, curry powder, chumvi na pilipili manga. Changanya vizuri, funika sufuria kwa dakika kama 5 au mpaka nyanya ziive vizuri. Funua sufuria, geuza nyanya
Hatua ya 4
Ongeza maharagwe na tui la nazi. Unaweza kuongeza na maji kiasi sana yakihitajika. Changanya vizuri kisha funika tena. Punguza moto yaive moto wa chini kwa dakika kama 3 mpaka 5, au mpaka sosi ichemke vizuri na iwe na uzito utakaopenda. Unaweza usiweke maji kama utaoenda iwe nzito sana
Hatua ya 5
Zima jiko. Ongeza majani ya giligilani na maji ya limao. Changanya vizuri
Hatua ya 6
Pakua ya moto na chakula utakachopenda

Comments
Join discussion.