Maini ya ng´ombe ni mboga rahisi na tamu kama utaipatia kupika, na pia unaweza kuyachukia endapo utakosea kuipika. Jaribu recipe yatu utupe mrejesho
Yaliyomo kwenye ukurasa huu:
Dakika 30 | Idadi ya walaji 4 | Rahisi |
Mambo ya kuzingatia
Maini ya ng´ombe ni tofauti na maini ya kuku. Maini ya ng´ombe siyo malaini kama ya kuku, hivyo huitaji muda zaidi kwenye kuyapika
Mafuta ni muhimu kwenye maini kama utataka yapendeze. Tumia mafuta mazuri kiafya kama Olive oil. Maini wakinyimwa mafuta hawapendezi
Kitunguu, pilipili hoho na karoti zinapendeza zikikatwa ukubwa unaokaribiana na ukubwa wa maini. katakata vipande vikubwa vikubwa vitakavyokaribiana na ukubwa wa vipande vya maini
Kaanga maini na mafuta, kitunguu saumu na tangawizi kwanza mpaka yakaribie kuiva ili viungo vikolee vizuri, mbogamboga weka mwishoni ili zisiive sana na kubadilika rangi na kuua virutubisho
Ongeza viungo utakavyopenda kama pilipili, majani ya giligilani na vinginevyo kuongeza radha
Muda wa kupika usiwe mrefu sana ukafanya yakawa magumu
Video
Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube
Mahitaji
Kilo 1 maini
Vijiko 4 vya chakula mafuta ya kupikia
Vijiko 2 vya chakula kitunguu saumu na tangawizi
Chumvi kwa kuonja
Pilipili manga kwa kuonja
Kijiko 1 cha chai binzari ya manjano
Kitunguu 1 kikubwa
Karoti 1 kubwa
Pilipili hoho 1/2 x 3 rangi tofauti
1/2 limao
Maelekezo hatua kwa hatua
Hatua ya 1
Andaa viungo; Menya na kukatakata maini vipande virefu virefu. Katakata kitunguu, pilipili hoho na karoti vipande vinavyokaribiana ukubwa wa maini. Visiwe vidogo sana wala vikubwa sana. Kamua na maji ya limao, weka pembeni
Hatua ya 2
Weka mafuta kwenye kikaango; yakichemka ongeza maini, kitunguu saumu na tangawizi, chumvi pamoja na pilipili manga. Changanya vizuri, kaanga kwa dakika kama 2 kisha ongeza binzari ya majano, endelea ukaanga mpaka rangi ya ubichi iishe na maini yakaribie kuiva
Hatua ya 3
Ongeza karoti, endelea kukaanga. Endapo utaona majimaji yanatokea kwenye maini usiogope. Yatoe na kijiko weka pembeni, yatatumika baadae
Hatua ya 4
Karoti zikianza kuiva na maini yakikaribia kuiva kabisa, ongeza kitunguu maji na pilipili hoho. Endelea kukaanga kwa dakika kama 2
Hatua ya 5
Ongeza yale maji uliyoyatoa awali pamoja na maji ya limao, changanya vizuri kisha ipua
Hatua ya 6
Pakua kama utakavyopenda


Comments
Join discussion.