Makange ya kuku wa kuchoma ni mboga tamu, yenye rangi za mbogamboga za kuvutia na pia nzuri kiafya endapo utatumia kuku wa kienyeji aliyechomwa.

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Dakika 20 Idadi ya walaji 4 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Kuku wa kienyeji ni mzuri kiafya kuliko wa kisasa. Kuku anatakiwa awe ameshachomwa na kuwa tayari kwa kula kwa sababu anawekwa mwishoni kwa muda mfupi sana kuchanganyikana na viungo vingine. Unaweza pia kutumia kuku wa kukaangwa badala ya kuchoma

Mbogamboga tofauti zinatakiwa zisipikwe zikaiva sana ili usiue virutubisho na pia kupata radha nzuri. Unaweza pia kutumia mboga za aina nyingine tofauti kama brokoli, koliflawa, maharagwe machanga, spinach, mchicha na kadhalika.

Sufuria au kikaangio kipana kama wok ni kizuri sana kwa kupika mboga za aina hii. Ukitumia sufuria ndogo au nyembamba zitabanana na hazitaiva vizuri. Pia ukitumia kikaangio au sufuria isiyochika chini (non stick) hauhitaji mafuta mengi katika upikaji kitu ambacho kinaongeza ubora wa mboga yako

Viungo tofauti vinaweza kuongezwa kutokana na matakwa ya mpishi na walaji. Unaweza kuongeza pilipili au viungo vyovyote ulivyonavyo

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

Kuku 1 wa kuchoma mkubwa
Nyanya 2 kubwa kiasi
Kitunguu maji 1 kikubwa
Karoti 1 kubwa
Pilipili hoho nusu x3 (nyekundu, njano na kijani)
3/4 kijiko cha chakula kitunguu saumu
3/4 kijiko cha chakula tangawizi
Vijiko 3 vya chakula mafuta ya kupikia
Chumvi na pilipili manga kwa kuonja
1/4 kikombe majani ya kotimiri

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Kwenye sufuria katika moto wa wastani, chemsha mafuta kisha ongeza kitunguu maji, kitunguu saumu na tangawizi. Pika mpaka harufu ya ubichi iishe na vituguu vilainike ila visiive sana vikakauka wala kubadilika rangi. Hakikisha unageuza mara kwa mara visishike chini

Hatua ya 2

Ongeza nyanya, chumvi na pilipili manga. Changanya vizuri kisha funika na mfuniko pika mpaka nyanya zilainike kabisa. Ikibidi geuza na ongeza maji wakati bado zinaiva ili zisikaukie kwenye sufuria

Hatua ya 3

Ongeza karoti na pilipili hoho kwa dakika kama dakika 2. Kuwa makini zisiive sana, zinapendeza zikiwa mbichimbichi

Hatua ya 4

Ongeza kuku, changanya vizuri kabisa kuku akolee viungo kote. Ongeza na maji kidogo sana ikibidi ili kuku asikauke sana awe na unyevunyevu wa sosi

Hatua ya 5

Pakua ya moto na chakula utakachopenda kama wali, ugali, chipsi, ndizi za kuchoma au kukaanga na kadhalika

Comments

Join discussion.