Makaroni ya nyama ya kusaga ni chakula cha asili ya Waitaliano ambacho kinatengenezwa na makaroni au tambi, nyama ya kusaga na viungo vingine mbalimbali. Ni rahisi sana kutengeneza na chakula ambacho ni rahisi kama una wageni wengi kuepuka kupika vyakula vingi tofauti

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Dakika 50 Idadi ya walaji 2 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Nyama ya kusaga ya ng´ombe ni kiungo muhimu sana katika hili pishi. Unaweza kutumia nyama ya kusaga ya aina nyingine, lakini ya ng´ombe inapendeza zaidi

Tambi zipo za aina nyingi sana kwa hiyo zinaiva katika muda tofauti kutokana na ukubwa, maumbo, na zilivyotengenezwa. Tumia utakazopenda. Usichemshe tambi zikaiva sana zikawa kama ugali, chemsha kutokana na maelekezo ya kwenye pakiti. Kila pakiti ya tambi ina maelekezo ya muda wa kuchemsha

Chemsha tambi na maji na chumvi peke yake kwanza kisha ndio uchanganye kwenye mchanganyiko wa nyama ikiwa tayari.

Viungo tofauti vinaweza kuongezwa kutokana na matakwa ya mpishi na walaji. Beef seasoning au beef cubes (radha ya nyama) inapendezesha chakula zaidi

Nyama haichemshwi kabla ya kupikwa. Kaanga kwanza na kitunguu maji na viungo vingine, itachemka ukiweka nyanya na maji.

Acha nyama ichemke muda mrefu moto wa chini. Hii itapendezesha chakula zaidi maana nyama itachanganyikana taratibu na vizuri zaidi na viungo vingine. Unaweza kuchemsha kwa dakika mpaka 40 kama muda unaruhusu

Kuchanganya nyama na tambi mwishoni hakuhitaji kuchemsha kwa muda mrefu. Ukichanganya vizuri, ipua na pakua tayari kwa kula. Kuwa muangaliafu usiache kwa muda mrefu makaroni yakapitiliza kuiva

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

250g/ robo kilo nyama ya kusaga
250g/ robo kilo makaroni
Kitunguu maji kimoja cha wastani
Nyanya 2
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu na tangawizi
Vijiko 3 vya chakula mafuta ya kupikia
Kijiko 1 cha chakula beef seasoning
Kikopo 1 nyanya ya kopo
Pilipili manga kwa kuonja
Chumvi ikihitajika
Jibini ya chaguo lako ya kunyunyizia juu (ukipenda)

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Saga nyanya na kitunguu maji kwenye mashine ya kusagia chakula kupata rojo. Ukipenda unaweza kukatakata vitunguu na nyanya vipande vidogovidogo badala ya kusaga

Hatua ya 2

Chemsha makaroni kulinganya na maelekezo ya kwenye pakiti, ipua dakika 2 kabla ya kuiva. Osha na maji ya baridi ili yasiendelee kuiva na kushikana, weka pembeni

Hatua ya 3

Kwenye sufuria katika moto wa wastani, chemsha mafuta. Ongeza nyama ya kusaga, beef seasoning, kitunguu saumu na tangawizi pamoja na pilipili manga. Endapo utakatakata kitunguu maji badala ya kusaga, unaweka katika hatua hii ili kiive na nyama. Kaanga kwa dakika kama 5, au mpaka nyama ianze kupata rangi ya kahawia

Hatua ya 4

Ongeza rojo ya nyanya na kitunguu (kama umekatakata itakuwa vipande vya nyanya peke yake). Koroga vizuri, funika na mfuniko. Acha nyama iive moto wa wastani kwa dakika kama 20, au mpaka iive vizuri na maji yakaukie

Hatua ya 5

Ongeza nyanya ya kopo na maji kama nusu kikombe. Funika tena, pika kwa dakika kama 10 mpaka 15; au mpaka sosi iwe nzito ila isikauke

Hatua ya 6

Ongeza makaroni kwenye mchanganyiko wa nyama na maji kidogo yakihitajika. Changanya vizuri pika kwa dakika 2 zilizobakia kwenye kuchemshia makaroni. Ongeza na chumvi kiasi ikihitajika

Hatua ya 7

Pakua na jibini kama utapenda

Comments

Join discussion.