Hii ni recipe ya kuku ambayo jirani zangu wote wanaomba nitengeneze kila tunapokuwa na sherehe au mikutano tofauti. Kuna watoto wa jirani pia wanaochukia nyama, wazazi wao wamenifata kuniambia hii ndiyo nyama pekee watoto wao wanakula. Ni rahisi kutengeneza, jaribu utupe majibu
Yaliyomo kwenye ukurasa huu:
Dakika 25 | Idadi ya walaji 4 | Rahisi |
Mambo ya kuzingatia
Minofu ya kuku ni nyama unayoipata kutoka kwenye kifua au sehemu ya juu ya mapaja ya kuku. Nyama ya mapaja ya kuku huwa ni laini zaidi kuliko ya kifua, lakini zote ni tamu na zinapendeza sana kwa recipe hii
Kukoleza viungo kwa kuacha kwenye friji usiku mzima kama una muda kunaongeza radha nzuri zaidi kwenye kuku. Kuku anayewekewa tangawizi na kitunguu saumu hulainika vizuri pia, kwa hiyo ukikaanga atakuwa crispy (kaukau) nje na mlaini ndani; ndiyo lengo letu kubwa
Viungo vinavyokosekana mahali ulipo mbali na kitunguu saumu na tangawizi vinaweza kubadilishwa. Unaweza pia kuongeza viungo vingine mbalimbali ambavyo unavipenda na umevizoea
Chenga za mkate au Bread Crumbs zinapatikana kwa wingi madukani na supermarkets. Ukiweza tumia zenye jina la PANKO, zinakuwaga nzuri zaidi. Ukikosa Panko tumia zinazopatikana
Moto wakati wa kukaanga usiwe mkali sana ukababua kuku nje akatoka mbichi ndani. Moto ukiwa mdogo sana pia kuku atanyonya mafuta na hatakauka vizuri. Hakikisha moto ni sahihi katika kukaanga
Usijaze sana kikaango acha kuku waive kwa nafasi na usawa. Kama una kikaango kidogo, pika kidogokidogo ila kuhakikisha wanaiva vizuri
Hakikisha mafuta yamechemka vizuri wakati unaweka kuku. Mafuta yasipochemka vizuri kuku atanyonya mafuta wakati wa kula utakinai na hutafurahia. Mafuta yasiyocheka pia yanafanya kuku asikauke vizuri
Tissues za jikoni au gazeti ni muhimu sana unapotoa kuku kwenye mafuta. Huu husaidia kufyonza mafuta yaliyobakia ili kuku asiwe na mafutamafuta wakati wa kula
Video
Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube
Mahitaji
500g/ nusu kg minofu ya kuku
Vikombe 2 vya chai chenga za mkate (Bread crumbs)
Vijiko 3 vya chakula unga wa ngano
Mayai 2
Kijiko 1 cha chakula tangawizi na kitunguu saumu
Chumvi na pilipili manga kwa kuonja
Mafuta ya kukaangia
Maelekezo hatua kwa hatua
Hatua ya 1
Osha, kausha na katakata minofu ya kuku vipande virefu vyembamba kiasi
Hatua ya 2
Kwenye bakuli kubwa, changanya vizuri vipande vya kuku tangawizi na kitunguu saumu; chumvi na pilipili manga. Funika bakuli, weka kwenye jokofu/ friji kwa muda wa nusu saa au mpaka masaa 24. Jinsi anavyoendelea kukaa ndiyo anavyozidi kupendeza
Hatua ya 3
Chemsha mafuta kwenye kikaangio moto wa juu kiasi. Wakati mafuta yanachemka, piga mayai kwenye bakuli. Weka unga wa ngano na chenga za mkate kwenye sahani tofauti pana iwe rahisi kuchovya
Hatua ya 4
Paka vipande vya kuku unga wa ngano, halafu chovya kwenye mayai yaliyopigwa na mwishoni zungushia kuku wako chenga za mkate. Kwa kutumia mkono, gandamiza chenga kwenye kuku zishike vizuri
Hatua ya 5
Weka kuku kwenye mafuta yaliyochemka, acha aive hadi awe na rangi ya kahawia na mkavu kwa juu. Unaweza kuongeza na kupunguza moto ikibidi
Hatua ya 6
Kuku akiiva, weka kwenye sahani yenye tissues za jikoni ili tissues zifyonze mafuta



Majadiliano
embedd discussion component here.
Comments
Join discussion.