Mlenda mkavu ni mboga ya majani ya kukaushwa na kusagwa inayoliwa na makabila mengi ya Tanzania. Kanda ya ziwa kwa wasukuma wanauita Mzubo, Wanyamwezi wanauita Nswalu, Iringa wanauita Mkunungu, Wanyiramba wanauita Ndalu, Wanyaturu wanauita Ighonda, Wapare wanauita Msele, Wagogo wanauita Lilende na kadhalika. Kwa kawaida mboga hii hupikwa kwenye chungu na kuchanganywa kwa mpekecho (kijiti maalum ca kukorogea) na kuwekewa karanga za kusaga kuongeza uzito na radha. Mlenda pia hauhitaji viungo vingi zaidi ya maji na chumvi pamoja na karanga za kusaga
DSC00975

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Dakika 10 Idadi ya walaji 4 Rahisi sana

Mambo ya kuzingatia!

Mlenda unaweza kununua sokoni au kwa wanaouza mboga za kukausha. Mara nyingi unauzwa bila kusagwa. Kiasili mlenda unatwangwa kwenye kinu na kuchekechwa kwenye chekecheo kuhakikisha umelainika vizuri. Lakini kutokana na teknolojia ya sasa, unaweza pia kusaga kwenye mashine tofauti za kusagia vyakula

Karanga za kusaga ni kiungo muhimu sana kwenye mlenda mkavu kwani huongeza radha na uzito. Unaweza kuongeza na kupunguza karanga kutokana na matakwa ya walaji. Kiasili, mlenda mkavu unawekewa karanga nyingi. Na pia nimetumia karanga ambazo zilikaangwa kabla ya kusagwa ndio maana sijapika kwa muda mrefu, unaweza pia kutumia karanga mbichi ila hakikisha umezichemsha zikaiva kabla ya kuweka mrenda

Maji ya moto ni muhimu kuanzia unaanza kupika na utakapokuwa unaongeza wakati wa kupika. Ukiweka maji ya baridi wakati mlenda unaiva jikoni inamaanisha maji yataupoza kwanza ndiyo yaanze kuuchemsha tena, inaweza kufanya mlenda ukadoda usichangamke

Chumvi ni vizuri kuweka kidogokidogo sana kwa sababu mlenda unashika sana chumvi. Na pia kumbuka kama unatumia karanga za kusaga za kopo mara nyingi zinakuwaga na chumvi iliyojitosheleza, unaweza usihitaji au ukaongeza kidogo sana

Koroga mara kwa mara mara baada ya kuweka karanga kwa sababu karanga zinashika chini kwa urahisi sana. Na pia kuwa muangalifu usipike na moto mkali sana kuzuia kushika chini na kuungua

Chungu kinafaa zaidi kupikia mlenda kuliko sufuria kama utakuwa nacho

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

1/2 Kikombe karanga za kusaga
Vijiko 2 vya chakula mlenda mkavu
Kikombe 1 maji ya kuanzia, na maji zaidi ya kuongezea
Chumvi kiasi kama itakavyohitajika

Maelekezo hatua kwa hatua

DSC00969

Hatua ya 1

Anza kwa kuweka maji ya moto na karanga za kusaga kwenye sufuria. Chemsha katika moto wa wastani huku unakoroga mara kwa mara ili karanga zisishike chini kwenye sufuria. Ongeza maji ya moto kodogokidogo huku unakoroga mpaka upate uzito unaoutaka. Acha zichemke zitokote kwa dakika kama 3, huku unaendelea kukoroga mara kwa mara

Hatua ya 2

Ongeza mlenda huku unakoroga haraka haraka kuzuia mrenda kupata mabonge. Endelea kuongeza na maji ya moto kidogokidogo endapo yatahitajika ili upate uzito utakaopenda

Hatua ya 3

Ongeza chumvi. Kumbuka chumvi unaweka kidogo sana kwa sababu mlenda unashika chumvi kwa haraka sana

Hatua ya 4

Endelea kuchanganya vizuri, ukipata uzito unaotaka, acha mlenda utokote moto wa wastani kwa dakika kama 3 mpaka 5 nyingine, au mpaka utakaporidhika kuwa umeiva vizuri. Kumbuka kugeuza mara kwa mara ili usishike chini kwenye sufuria

Hatua ya 5

Pakua na ugali wa muhogo, dona au ugali mwingine wa aina yoyote. Enjoy

C0142T01

Comments

Join discussion.