Hii ni recipe rahisi sana hata kwa ambao hawajawahi kuoka kabisa au wanaopenda kuoka na watoto. Hauhitaji mashine yoyote kwenye kuchanganya na unahitaji kama nusu saa kutengeneza kila kitu. Kwa wazazi wenye watoto wanaokwenda shule, cupcakes za ndizi zinafaa sana kuweka kwenye snack box

3o dakika Idadi 18 Rahisi

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Mambo ya kuzingatia

Siagi ni lazima iyeyushwe kabla ya kutumia. Kwa sababu haitumii mashine, matumizi ya siagi iliyoyeyuka kabisa ni muhimu sana. Inaweza kuyeyusha kwenye microwave, sufuria kwenye jiko au ndani ya bakuli kisha uweke bakuli kwenye maji ya moto. Hakikisha haipati moto, iyeyuke tu na iwe na joto la kawaida

Sukari inaweza kupunguzwa au kutokuwekwa kabisa kwa wanaooka kwa ajili ya watoto wadogo au wasiopenda sukari. Kumbuka ndizi ni tamu sana tayari, ukipunguza sukari bado utapata utamu wa kutosha

Baking powder na baking soda zina matumizi tofauti katika uokaji. Katika recipe hii unahitaji zote, baking powder na baking soda

Kuchanganya sana kunaharibu na kufanya cupcakes zisilainike vizuri. Ukiweka mchanganyiko wa unga wa ngano na viungo vikavu, changanya tu kuhakikisha hakuna weupe weupe na viungo vimechanganyikana vizuri, usizidishe zaidi ya hapo

Kwenye kuoka, ili kupata cupcakes nzuri hakikisha umewasha oven na imepata joto kabla ya kuoka. Pia hakikisha oven imewasha kwenye setting ya joto la juu na chini. Pia tumia joto kama kwenye maelekezo, usiweke moto mkali sana zikababuka au wa chini sana zikadorola

Hifadhi kwenye air tight container kwa siku moja nje ya friji au ndani ya friji kwa siku 5 mpaka 6. Unaweza pia kuzigandisha kwenye freezer mpaka miezi 3

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

Vikombe 1-1/2 unga wa ngano
Kijiko 1 cha chai baking powder
1/2 kijiko cha chai baking soda
1/4 kijiko cha chai chumvi
1/2 kikombe siagi iliyoyeyushwa
1/2 Kikombe sukari
Kikombe 1-1/2 ndizi za kuponda (kama dizi 4 za wastani)
Mayai 2 makubwa
1/2 kijiko cha chai vanilla extract

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Anza kwa kuwasha oven joto la 170 degrees C ili ipate joto wakati unachanganya unga. Panga karatasi za cupcakes kwenye chombo cha kuokea. Endapo hauna karatasi, basi paka mafuta chombo cha kuokea, weka pembeni.

Hatua ya 2

Changanya unga wa ngano, baking powder, baking soda na chumvi kwenye bakuli. Ikichanganyika vizuri, weka pembeni

Hatua ya 3

Ponda ndizi kwa kutumia uma, mwiko au kifaa chochote rahisi kwako mpaka zilainike vizuri; usitumie mashine tumia mkono, weka pembeni. Ndizi zikiwa tayari, ongeza siagi, sukari, mayai na vanilla kwenye bakuli lenye ndizi. Changanya mpaka uchanganyiko uchanganyikane vizuri kabisa

Hatua ya 4

Ongeza mchanganyiko wa unga wa ngano kwenye bakuli la mchanganyiko wa ndizi. Changanya mpaka tu uchanganyike vizuri. Haifai uchanganye sana, ukichanganya sana cupcakes hazitachambuka vizuri. Tumia tu mwiko au kijiko cha kuchanganyia kuchanganya kwa dakika chache.

Hatua ya 4

Gawanya mchanganyiko kwenye vikopo 12 mpaka 18 vya kuokea muffins vilivyojazwa ujazo wa robo tatu; visijae sana wala visiwe na unga kiasi sana

Hatua ya 5

Oka kwa dakika 18 mpaka 22, au mpaka ukichomeka kijiti kitoka kisafi

Hatua ya 6

Ipua, acha zipoe kwa dakika 5 kwenye chombo cha kuokea kabla ya kuhamishia kwenye waya wa kupozea zipoe kabisa

Hatua ya 7

Enjoy

Comments

Join discussion.