Nyama ya kukaanga na mbogamboga ni moja ya mboga rahisi sana kupika, yenye virutubisho vingi na haihitaji muda mrefu kuipika
Yaliyomo kwenye ukurasa huu:
Dakika 20 | Idadi ya walaji 2 | Rahisi |
Mambo ya kuzingatia
Kikaango au Sufuria pana inafaa zaidi kwa pishi hili. Nyama na mbogamboga vyote vinapendeza kuiva kwa nafasi. Ukiweza tumia frying pan aina ya WOK, ni nzuri sana kwa mapishi ya vyakula vya kukaanga
Mbogamboga zinapendeza zaidi zikipikwa bila kuiva sana. Unaweza kutumia mbogamboga za aina yoyote utakazopenda wewe kama brokoli, koliflawa, maharagwe machanga na kadhalika
Nyama sahihi ni ile steki inayouzwaga kwa ajili ya kukaanga. Nyama hii huiva haraka sana na ni laini pia. Ukienda supermarkets ulizia ribeye, entrecote, flank steak, Tenderloin Steak, Round Steak, Sirloin Steak na kadhalika. Ukitumia nyama ya kawaida haitaiva na kuwa laini kama zilizoorodheshwa hapo juu
Kaanga nyama kidogokidogo endapo kikaango chako ni kidogo. Usijaze sana, hakikisha zimesambaa hazibebani ili ziive kwa usawa bila kupishana. Kumbuka usipike nyama muda mrefu ikakauka utaharibu radha, dakika kama 3 kwa pande zote zinatosha
Pakua ya moto mara baada ya kuipua. ikipoa haitapendeza sana
Unaweza kula na wali, ugali, chipsi, ndizi za kuchoma au kukaanga au chakula chochote utakachopenda
Video
Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube.
Mahitaji nyama na mbogamboga
400g steki laini ya nyama
Vijiko 4 vya chakula mafuta ya kupikia
Hoho nusu x3; rangi mchanganyiko
Kitunguu maji 1
Karoti 1 kubwa
1/2 kikombe kitunguu cha majani
Chumvi na pilipili manga kwa kuonja
Pilipili kichaa 2 (ukipenda)
Majani ya giligilani kiasi (ukipenda)
Mbegu za ufuta (ukipenda)
Mahitaji ya sosi
Vijiko 3 vya chakula soy sauce
Kijiko 1 cha chai kitunguu saumu
Kijiko 1 cha chai tangawizi
Kijiko 1 cha chakula maji ya ndimu
Kijiko 1 cha chakula sukari
Maelekezo hatua kwa hatua
Hatua ya 1
Ondoa mbegu kwenye hoho halafu uzikatekate pamoja na karoti na kitunguu maji vipande vyembamba virefu. Katakata pilipili, majani ya kitunguu na majani ya giligilani; Katakata nyama vipande virefu; Twanga kitunguu saumu na tangawizi; kamua maji ndimu
Hatua ya 2
Katika bakuli dogo, changanya soya sosi, sukari, maji ya ndimu, kitunguu saumu na tangawizi. Weka pembeni.
Hatua ya 3
Kwenye kikaangio katika moto mkali weka vijiko viwili vya mafuta ya kupikia. Yakichemka ongeza nyama. Isambaze kwenye kikaangio isibebabe
Hatua ya 4
Geuza upande wa pili. Ongeza chumvi na pilipili manga. Kaanga nyama mpaka iive kama utakavyopenda. Hamishia nyama kwenye sahani, weka pembeni
Hatua ya 5
Kwenye kikaango hichohicho, punguza moto uwe mkali wastani. Ongeza vijiko viwili vya mafuta halafu uweke kitunguu maji kwa sekunde chache; kisha ongeza karoti. Pika kwa dakika kama 2. Ongeza pilipili hoho, kaanga ziive kama utakavyopenda wewe
Hatua ya 6
Ongeza nyama, majani ya kitunguu na pilipili kichaa, kaanga kwa sekunde chache halafu mimina mchanganyiko wa sosi. Changanya vizuri kwa dakika kama 1
Hatua ya 7
Ongeza majani ya giligilani, changanya; nyunyizia mbegu za ufuta kwa juu endapo utatumia



Comments
Join discussion.