Pizza ni chakula cha asili ya waitaliano kinachopendwa na watu wengi duniani. Mbali na ubora na utamu wa pizza, vilevile ni chakula rahisi sana kutengeneza kuliko wengi wanavyofikiria. Pizza inapendeza zaidi ukiitengeneza mwenyewe na viungo unavyopenda wewe

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Dakika 45 Idadi ya walaji 4 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Vipimo ni muhimu katika uokaji wa pizza. Kama unataka matokeo mazuri, fuatilia vipimo kama vilivyo, kamwe usikadirie chochote. Tumia vikombe na vijiko maalum kwa kupimia ili kupata matokea mazuri zaidi

Hamira ni kiungo muhimu katika pizza. Hakikisha hamira yako haijakaa muda mrefu kabla ya kutumia na pia pima sahihi kama inavyohitajika

Maji ya uvuguvugu ni muhimu katika uumuaji wa mkate wa pizza. Hakikisha siyo yamoto sana ya kuunguza hamira au ya baridi ya kufanya isiumuke vizuri

Mozarella cheese ndiyo sahihi kwa pizza na inapatikana kwa wingi supermarkets. Kuna sehemu nyingine unaweza kukuta cheese maalum kwa ajili ya pizza, unaweza kutumia hiyo pia

Chombo cha kuokea tumia mahususi kwa ajili ya pizza, usipokuwa nacho tumia karatasi za kuokea. Weka karatasi kwenye chombo chochote cha kuokea ndiyo uweke pizza kwa juu. Ukitumia chombo cha kawaida bila karatasi kumbuka kupaka mafuta ili kupata matokeo mazuri sana

Kuoka pizza hakikisha umewasha oven moto wa juu na chini na oven imepata joto kabla ya kuweka kwenye oven. Pizza inaokwa kwa moto mkali sana, ukiweka moto wa chini itadoda

Kuoka sahihi na kupata pizza nzuri, anza kwa kuwasha oven moto wa juu na chini, oven ikipata moto ukiweka pizza badilisha joto liwe la chini peke yake kwa dakika 10, kisha weka moto wa juu na chini kwa dakika kama 3 mpaka 5 nyigine. Hii inasaidia viungo vya juu kama cheese na mbogamboga visiive kupitiliza

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

Pakiti 1 au kijiko 1 cha chakula hamira
Kijiko 1 cha chai sukari
Kikombe 1 maji ya uvuguvugu
Vikombe 2-1/2 unga wa ngano
Kijiko 1 cha chai chumvi
Vijiko 2 vya chakula olive oil

Mahitaji ya viungo vya juu

250g mozarella cheese
1/2 kikombe tomato sauce ya pizza
Viungo vingine utakavyopenda (nyama, uyoga, vegetables, n.k)

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Washa oven joto la 250 degrees C. Acha ipate moto wakati unaandaa unga

Hatua ya 2

Changanya maji ya uvuguvugu, sukari na hamira kwenye bakuli kubwa. Funika bakuli na kitambaa kisafi, acha hamira iumuke kwa dakika kama 5-10

Hatua ya 3

Hamira ikiumuka, ongeza unga wa ngano, chumvi na olive oil. Kanda unga mpaka ulainike vizuri. Funika tena bakuli, acha unga uumuke kwa dakika kama tano

Hatua ya 4

Gawanya unga madonge mawili (au zaidi kutokana na ukubwa wa pizza unaotaka). Sukuma kwenye sehemu uliyomwahia unga wa ngano. Ukisukuma nyembamba, izidi unene chapati kidogo sana inapendeza zaidi kuliko ukifanya nene sana.

Hatua ya 5

Weka unga wa pizza kwenye chombo cha kuokea ulichoandaa. Kama una chombo special cha pizza au unatumia karatasi za kuokea kwenye chombo chochote cha kuokea

Hatua ya 6

Ongeza tomato sauce ya pizza. Sambaza vizuri kisha mwagia mozarella cheese kwa juu, isambaze vizuri pia. Ongeza viungo vilivyobakia ulivyoamua kutumia kwa juu

Hatua ya 7

Oka pizza kwa dakika kama 13-15. Anza kwa kuoka moto wa chini peke yake ili iwe crispy chini na viungo vya juu visiungue sana. Oven ikishapata moto, badilisha setting weka moto wa chini peke yake ndiyo uweke pizza ndani. Oka kwa dakika 10 kisha badilisha weka moto wa juu na chini, oka kwa dakika kama 3 mpaka 5 kisha ipua

Hatua ya 8

Acha ipoe kiasi kwa dakika kama 5 kabla ya kuliwa. Katakata na pakua kama utakavyopenda. Enjoy

Comments

Join discussion.