Kwenye vyakula kuna baadhi ya vyakula haviendi bila kachumbari au salad. Fikiria pilau au biryani kwa mfano uile bila kachumbari, hainogi kabisa. Mbali ya hapo kuna kachumbari za aina nyingi tofauti zinazohitaji viungo tofauti. Leo nawaletea kachumbari rahisi na tamu sana, pia nzuri sana kiafya. Kachumbari hii inajulikana kama Raita kwa watu wa India. Kuna raita za aina tofauti pia, tuanze na hii leo.....next time tujaribu nyingine
DSC00344-2

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Dakika 20 Idadi ya walaji 4 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

DSC00324
Greek yogurt ni nzito zaidi kwa hiyo inapendeza zaidi kwenye kutengeneza hii kachumbari. Au tumia maziwa yoyote ya mgando. Kwa matokeo mazuri zaidi, tumia full cream yogurt

Tango ndiyo kiungo cha muhimu kwenye hii kachumbari. Tumia tango fresh kupata radha nzuri zaidi

Usafi ni muhimu sana kwenye utengenezaji wa kachumbari. Tumia kibao cha kukatia kuepuka kushikashika sana viungo. Pia tumia kitambaa kisafi kuchuja tango

Majani ya coriander na mint ndiyo chachu ya recipe hii. Tumia fresh kabisa ambayo hayajasinyaa. Unaweza pia kuongeza au kupunguza vipimo vya majani kupata radha itakayokufurahisa

Vipimo vinaweza kubadilishwa pia ili kupata radha utakayopenda. Ongeza na kupunguza maziwa ya mgando kwa mfano, majani ya coriander na majani ya mint.

Viungo vya ziada kama paprika, binzari ya pilau, pilipili ya kukausha na kadhalika vinaweza kuongezwa ili kupata radha nzuri zaidi

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

Tango 1
Limao 1
1/4 kikombe majani ya mint
1/2 kikombe majani ya mint
1/2 kikombe maziwa ya mgando
Chumvi kama itakavyohitajika
Pilipili manga kama itakavyohitajika

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Kamua maji ya limao. Osha majani ya coriander na mint

Hatua ya 2

Weka majani ya coriander, mint pamoja na maji ya limao kwenye mashine, saga mpaka yalainike vizuri kabisa

Hatua ya 3

Osha, menya na kukwangua tango kwenye grater; tumia matundu makubwa kabisa ya grater

Hatua ya 4

Kamua maji ya kwenye tango kwa kutumia kitambaa safi cha jikoni. Maji yanasababisha kachumbari iwe na majimaji sana isipendeze
C0376T01

Hatua ya 5

Weka tango kwenye bakuli safi. Ongeza maziwa ya mgando, chumvi, pilipili manga pamoja na mchanganyiko wa limao na majani. Weka mchanganyiko wa limao na majani kidogokidogo sana huku ukionja mpaka upate radha itakayokuridhisha. Mimi napenda kuweka nusu kijiko kwa nusu kijiko mpaka niridhike. Unaweza pia kuongeza na kupunguza maziwa ya mgando kama utakavyopenda
DSC00305

Hatua ya 6

Funika bakuli, weka kwenye friji kwa dakika kama 15 kama muda utaruhusu. Kama muda hauruhusu unaweza kuila kachumbari mara baada ya kuitengeneza

Hatua ya 7

Enjoy na chakula chochote kitakachokufurahisha. Inapendeza sana na pilau, biryani, wali wa viungo, mihogo au ndizi choma/ kaanga na kadhalika
introojpg-3

Comments

Join discussion.