Dagaa ni mboga inayopendwa sana na watu wengi. Dagaa ukikosea kuwapika utawachukia, lakini ukiwapika vizuri hutawachoka. Jaribu recipe yetu utupe mprejesho
Yaliyomo kwenye ukurasa huu:
Dakika 30 | Idadi ya walaji 4 | Rahisi |
Mambo ya kuzingatia
Dagaa wapo wa aina nyingi. Chagua dagaa unaowapenda wewe. Recipe hii inafaa kwa dagaa wa aina zote
Mafuta ni muhimu kwenye dagaa kama utataka wapendeze. Tumia mafuta mazuri kiafya kama Olive oil. Dagaa wakinyimwa mafuta hawapendezi
Kitunguu, pilipili hoho na karoti zinapendeza zikikatwa ukubwa unaokaribiana na ukubwa wa dagaa. Dagaa wadogo vipande vidogo, wakubwa vipande vikubwa
Kaanga dagaa kwenye kikaango kabla ya kuwaosha ili kama wana michanga itoke kiurahisi. Kuwakaanga pia inasaidia wakauke vizuri wasiwe rojorojo
Toa vichwa na osha dagaa mara kadhaa kama ni wale wenye michanga. Dagaa wasafi hawahitaji kutolewa vichwa wala kuoshwa mara nyingi
Kaanga dagaa na kitunguu na mafuta mpaka wakauke vizuri kabla ya kuweka nyanya na viungo vingine
Video
Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube
Mahitaji
Vikombe 2 dagaa
Vijiko 3-4 vya chakula mafuta ya kupikia
Chumvi kwa kuonja
Kijiko 1 cha chai binzari ya manjano
Kitunguu 1 kikubwa
Nyanya 2 za wastani
Karoti 1 ya wastani
Pilipili hoho 1/2
Maji kiasi
Maelekezo hatua kwa hatua
Hatua ya 1
Andaa viungo; katakata kitunguu, nyanya, pilipili hoho na karoti vipande vinavyokaribiana ukubwa na dagaa. Visiwe vidogo sana wala vikubwa sana
Hatua ya 2
Kaanga dagaa kwenye sufuria bila mafuta wala kitu kingine chochote kwa dakika chache, kisha hamishia kwenye bakuli. Ongeza maji ya moto kwenye bakuli. Waoshe dagaa, chuja maji, weka pembeni
Hatua ya 3
Kwenye sufuria au kikaango katika moto wa juu kiasi, weka mafuta. Ongeza kitunguu maji, kaanga kwa dakika chache. Kuwa muangalifu kitunguu kisikauke wala kubadilika rangi, kiive tu kiasi
Hatua ya 4
Ongeza dagaa waliooshwa. Kaanga huku unageuza mpaka dagaa wakauke. Usikoroge sana wakabondekabondeka. Kama mafuta hayatatosha, unaweza kuongeza kiasi.
Hatua ya 5
Ongeza chumvi na binzari ya manjano. Endelea kukaanga mpaka dagaa wakauke vizuri kabisa
Hatua ya 6
Ongeza nyanya na karoti. Acha viive kiasi, kisha geuza. Endelea kuacha viive kidogo kisha unageuza mpaka nyanya ziive vizuri na zichanganyikane vizuri na dagaa. Kwa wapenzi wa pilipili, unaweza kuongeza pilipili pia
Hatua ya 7
Ongeza pilipili hoho. Changanya kwa dakika 1 au 2, kuwa muangalifu pilipili hoho zisiive sana zikabadilika rangi. Zinapendeza zikiwa na rangi nzuri ya kijani na zisiwe laini sana
Hatua ya 8
Ongeza maji kiasi kama utataka kamchuzi kidogo. Pakua na enjoy






Comments
Join discussion.