Recipe rahisi ya nyama ya mbuzi yenye viungo vinavyosaidia kukata harufu ya mbuzi. Inafaa kuliwa na chakula cha aina yoyote, iwe kama rosti ya biryani kwa siku maalum au mboga ya kulia ugali na wali kwa siku za kawaida

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Saa 1 Idadi ya walaji 4 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Marinate nyama usiku kucha, inapendeza zaidi na pia inakuwa rahisi kulainika wakati wa kupika. Unaweza ukaandaa mpaka siku 2 kabla ya kupika. Unaweza pia kumarinate nyama kisha ukaiweka kwenye freezer kwa muda mrefu zaidi

Viungo vizima vinasaidia kuongeza radha iwe nzuri sana kwenye nyama. Ongeza na kupunguza viungo kutokana na matakwa ya mpishi na walaji

Maziwa ya mtindi yanapendeza zaidi yakiwa full cream kuliko low fat. Ila mwishoni ni mapenzi ya mpishi na walaji

Pika muda mrefu zaidi kama nyama itachelewe kulainika. Ongeza maji mpaka ilainike vizuri

Majani ya giligilani yawekwe mwishoni kabisa wakati unaipua nyama kwenye moto kwa sababu yanalainika kwa haraka sana

Kula nyama na vyakula vya aina tofauti kama wali, ugali, biryani, chapati, naan bread, mkate na kadhalika

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji ya nyama

Kilo moja nyama ya mbuzi
Vijiko 2 vya chakula kitunguu saumu na tangawizi
Vijiko 3 vya chakula mafuta ya kupikia
Chumvi kwa kuonja
Pilipili manga kwa kuonja

Mahitaji ya rosti

Vijiko 2 vya chakula mafuta ya kupikia
Punje 5-8 za karafuu
Punje 5-8 za iliki
Bay leaves 2-3
Kipande cha mdalasini
Pilipili manga nzima kama 10
Vitunguu maji 4 vya wastani
Chumvi kwa kuonja
Kijiko 1 cha chai binzari ya manjano
Vijiko 2 vya chai coriander powder
Nyanya 4 za wastani
Kijiko 1-1/2 garam masala
3/4 kikombe maziwa ya mgando
Majani ya giligilani au kotimiri

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Anza kwa kumarinate nyama. Unaweza kuandaa usiku halafu upike kesho yake mchana au jioni, nyama itapendeza zaidi. Weka nyama, paste ya kitunguu saumu na tangawizi, chumvi na vijiko 3 vya mafuta kwenye bakuli kubwa au mfuko. Changanya vizuri, weka kwenye friji mpaka siku 2. Inavyozidi kukaa ndiyo inazidi kupendeza

Hatua ya 2

Ukiwa tayari kupika, toa nyama kwenye friji. Andaa viungo; katakata kitunguu, nyanya na majani ya giligilani, weka pembeni

Hatua ya 3

Weka vijiko 2 vya chakula kwenye kikaango au sufuria katika moto wa chini, yakichemka ongeza iliki, karafuu, mdalasini, pilipili manga na bay leaves. Pika moto wa chini kwa dakika kama 2. Ongeza moto uwe wa wastani, kisha ongeza kitunguu maji; kaanga mpaka kitunguu kianze kulainika

Hatua ya 4

Ongeza chumvi, coriander powder na binzari ya manjano, endelea kukaanga mpaka kitunguu kilainike na kianze kupata rangi ya kahawia kwa mbali. Ongeza nyama, endelea kukaanga mpaka rangi ya ubichi itoke kwenye nyama na pia nyama ikauke kiasi

Hatua ya 5

Ongeza nyanya, garam masala na maziwa ya mgando. Changanya vizuri, funika acha nyama iive katika moto wa wastani kwa dakika kama 20-30; au zaidi ukipenda. Unaweza kuongeza maji endapo nyama itakaukia kabla ya kuiva na kulainika vizuri. Baada ya dakika 20-30 funua nyama. Unaweza kutoa maganda ya nyanya kutokana na ulivyoikata

Hatua ya 6

Nyama ikiiva na kulainika vizuri, na kama umeridhika na uzito wa rosti yake, ongeza majani ya giligilani na ipua nyama jikoni

Hatua ya 7

Pakua ya moto na chakula utakachopenda

Comments

Join discussion.