Tunaishi kwenye jamii inayotufundisha kwamba kuwa na familia ni mojawapo ya mafanikio makubwa sana katika maisha ya binadamu. Hii imefanya kuwa na familia iwe mojawapo ya ndoto kubwa kwa watu wengi. Endapo utafanikisha ndoto hiyo, utapongezwa sana na kuonekana kuwa mtu uliyekamilisha jambo muhimu sana katika maisha yako. Haijalishi umri, jinsia, kipato, kabila, rangi ya ngozi, unapotoka na kadhalika, ukifikia umri fulani katika maisha yako, utaulizwa maswali mengi sana kuhusu mipango yako ya kuoa au kuolewa na lini unapanga kuanzisha familia. Ingawa kuwa na familia ni jambo muhimu kwa wengi, kuna baadhi ya watu wachache ambao wana mtazamo tofauti kuhusu kuwa na familia. Hii inaweza kusababishwa na kazi wanazofanya, aina ya maisha wanayotaka kuishi, matatizo ya kiafya, kutokuamini watu na kadhalika.

Ingawa kuwa na familia ni jambo kubwa la kheri, mara nyingi tunasahau kujipanga na kujiandaa vizuri na changamoto zinazoweza kuambatana na maamuzi yako. Usipokuwa muangalifu katika maandalizi unaweza kukutana na changamoto zinazoweza kukuweka katika wakati mgumu kisaikolojia na kiuchumu kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kinaweza kuathiri malezi ya mtoto. Siku zote jinsi unavyomlea mtoto wako angali tumboni, inachangia kwa kiasi kikubwa sana kwa mtoto kuwa mtu wa aina gani atakuwa akikua.

Katika ukurasa huu, tutajadili pamoja safari ya maandalizi ya kuongeza familia kuanzia ujauzito mpaka kujifungua na malezi ya mtoto; changamoto unazoweza kupitia na vilevile malezi ya mtoto hatua kwa hatua kutokana na umri

IMG_1040

Mambo ya kuzingatia kabla ya kuwa na familia

Kwa leo tutaanza na mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuanzisha familia. Kwa mtazamo wangu na kutokana na uzoefu mdogo niliopitia, nadhani kabla ya kuwa na familia au mtoto/ watoto, ni vizuri kujibu maswali yafuatayo

1. Je wewe kama wewe upo tayari kuwa mzazi?
Mara nyingi sana inatokea kuwa wazazi wetu au ndugu na marafiki wa karibu wanakuwa na ushawishi wa hali ya juu unaotupelekea kufanya maamuzi ya haraka ya kupata watoto bila kufikiria ni majukumu makubwa kiasi gani yanatusubiri mbeleni. Kuna wakati unakuta rafiki zako wote, ndugu wa tumbo moja, majirani mliokuwa wote, wafanyakazi wenzako, binamu wa kila upande na watu wengi wa umri wako wana wake/ waume na watoto tayari. Siku hizi na maisha ya mitandaoni unaweza kuona watu wengi unaowajua wanapiga picha nzuri na watoto wao kitu kinachoweza kukuletea shinikizo la rika (peer pressure). Kabla ya kuongeza familia, fikiria kwa makini je wewe kama wewe binafsi upo tayari au kuna sababu nyingine zinakuharakisha.

2. Una uwezo wa kifedha?
Ingawa watoto ni baraka, watoto pia wanakuja na changamoto zao na gharama kubwa ambazo usipokuwa muangalifu na kujipanga mapema, unaweza kujiweka kwenye wakati mgumu. Watoto wanahitaji chakula, malazi, mavazi, vifaa vya kuchezea, ada ya shule, safari za mara kwa mara kwa daktari na mambo mengine mengi ambayo huwezi kutegemea. Inaleta raha sana kujua mtoto wako yupo salama na hauna hofu ya kufikiria atakula nini kesho au akiugua sasa hivi nitalipaje matibabu yake. Kwa upande wangu, naona hakuna kitu kinauma mzazi kama kutokuwa na uwezo wa kumpatia mtoto wako mahitaji muhimu. Kabla ya kuwa na mtoto, weka kichwani kwako kuwa ukishamleta duniani huwezi kumrudisha popote. Anakuwa wajibu wako mpaka utakapomaliza safari yako ya mwisho. Je wewe umejiandaaje? Upo tayari? Una kazi au biashara inayoweza kukutosheleza wewe na familia unayotaka kuianzisha?

3. Upo na mtu sahihi kuwa mzazi mwenzako?
Ujauzito, kujifungua na malezi ya mtoto yanahitaji wazazi wote wawili. Hakuna kazi ngumu duniani kama ya kulea mtoto. Ingawa unaweza kupata msaada wa dada wa kazi, ndugu au wazazi wako; je mzazi mwenzako yupo tayari kuwa na mtoto/ watoto? na ikitokea hayupo tayari, umejiandaaje? na ikitokea leo umepata maradhi au haupo tena duniani, unadhani mzazi mwenzako ni mtu atakayeweza kulinda mtoto/ watoto wako na kuhakikisha anakua/ wanakua vizuri na salama? au ni nani utakayemuachia jukumu la kulea mtoto/ watoto wako? na unamuamini vipi?

IMG_1649-2

4. Upo tayari kubadilisha mfumo wako wa maisha?
Kuwa peke yako au na mwenza wako ni rahisi sana. Unaishi maisha huru na unaweza kufanya chochote bila kufikiria sana. Unaweza kuwa mtu unapenda kwenda out, kusafiri, fashion, unapenda sana kazi yako au hata tu utulivu ukiwa nyumbani; umejiandaaje na ujio wa mtoto? Mtoto akija katika maisha yako kila kitu kinabadilika. Hakuna safari za bila kupanga; hakuna kutoka sana out; kazini unakuwa hauna uhuru sana au hata tu ukimya na kulala kwa amani unabadilika. Unadhani itakuwa rahisi kwako kubadilisha mfumo wako wa maisha?

IMG_0950-1

5. Utafanyaje wakiwa mapacha?
Safari ya kupata mtoto inaweza kubadilika na kuwa safari ya kupata watoto. Unaweza ukawa umejipanga kupata mtoto mmoja wakaja wawili bila kutegemea. Je umejiandaaje? utaweza kuwatunza wote wawili?

6. Una msaada wa kutosha?
Kupata mtoto hasa kwa mama inamaanisha kuchukua likizo ndefu ya kazi, biashara, masomo au shughuli zozote unazofanya. Hata kwa wamama wa nyumbani wasiofanya kazi, inamaanisha utakuwa na kiumbe mdogo dhaifu anayekutegemea katika kila kitu. Mtoto anaongeza majukumu kila upande. Umejipangaje? Utakaa na mtoto wako kwa muda gani? Lini unapanga kurudi kwenye kazi au shughuli zako? na vipi ikitokea mambo yasiwe kama unavyotegemea? Ni msaada wa aina gani unaotegemea na kutoka kwa nani? na hao watu wapo tayari kukusaidia kwa kiasi gani?

7. Unapenda usingizi kiasi gani?
Najua hii itakuja kama utani lakini ni muhimu sana kwa wanaopenda kulala. Kwa mimi binafsi mara ya mwisho nimelala tarehe 1.06.2018....baada ya hapo nilikuwa labor masaa 21, baada ya kuzaliwa mwanangu sijalala tena zaidi ya masaa 6 kwa siku. Nilipenda sana kulala, sasa hivi mpaka mwili umeshazoea kutokupata usingizi. Je, unadhani unaweza kuishi maisha ya kutokulala kabisa kwa ajili ya kulea mtoto

Kila binadamu ana maamuzi yake binafsi na mipango tofauti ya maisha. Chochote nilichoandika juu ni maamuzi yangu na mipango yangu binafsi, haimaanishi ndiyo sahihi kwa kila mtu. Tujadiliane pamoja, acha comment chini tusikie zaidi kutoka kwako

Jiunge na mjadala.

Weka comment yako hapa