Sambusa ni kitafunwa maarufu sana nchini Tanzania na Kenya. Ni kitafunwa ambacho unakutana nacho kila mahali; kwenye sherehe na mikutano mbalimbali, mashuleni na maofisini, mahotelini na vibandani.....kila kona unazipata. Ingawa ni maarufu sana, sambusa pia zina changamoto katika upikaji wake, na ni ngumu kwa baadhi ya watu katika pishi lake. Tumezoea sana kuona sambusa za manda za kuchoma kulinganisha na manda za siagi zisizohitaji kuchoma ambazo upatikanaji wake ni wa nadra. Leo basi ninaandaa sambusa nzuri sana, laini kwa ndani na zimekauka vizuri kwa nje. Hizi ni sambusa zinazotengenezwa sana nchini India na pia ni rahisi kutengeneza kwa mtazamo wangu, kulinganisha na sambusa tulizozizoea kila siku
DSC00240

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Masaa 2 Idadi ya sambusa 16 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Ukandaji wa unga ni rahisi sana. Cha msingi ni kuhakikisha umechanganya siagi na unga wa ngano mpaka mchanganyiko uwe chengachenga vizuri. Kwenye ukandaji pia anza kwa kuweka maji 3/4 ya kikombe kisha ongeza kidogokidogo yaliyobakia mpaka upate donge zuri. Endapo maji yatazidi, usiogope. Ongeza unga kidogokidogo mpaka unga uache kunata

Nyama ya kusaga unaweza kutumia ya aina yoyote kama ya ngĀ“ombe, mbuzi, kuku, kitimoto na kadhalika. Zingatia muda wa kupika nyama kwa mfano kuku anaiva haraka na kitimoto kinahitaji muda zaidi kuua minyoo

Viungo nya nyama ya kusaga vinaweza kuongezwa na kupunguzwa kutokana na mapenzi ya mpishi. Unaweza ongeza viungo vikavu kama paprika, binzari tofauti au pilipili ya kukausha. Viungo kama pilipili fresh na mbogamboga tofauti zinaweza pia kuongezwa

Mapishi ya nyama ni rahisi sana, ila kuwa makini kwenye utumiaji wa pilipili hoho. Ukiziweka wakati nyama bado ya moto zinaweza kuweka majimaji kwenye nyama yanayoweza kusababisha changamoto kwenye ukunjaji na uchomaji ya sambusa. Hakikisha unaziweka mwishoni wakati nyama imeshapoa kabisa

Mafuta kwenye nyama hayahitajiki. Kumbuka mara nyingi nyama ya kusaga inakuwa na mafuta ambayo yanatosha kuwivishia nyama. Tumia non stick pan kuepuka nyama kushika chini. Endapo utatumia sufuria ya kawaida, tumia mafuta kiasi kuepuka nyama kushika chini

Ukunjaji wa sambusa ni rahisi sana. Kunja kama sambusa za kawaida. Kumbuka pia manda ambazo hazijachomwa zinaweza kugandishwa vizuri zaidi kwenye ncha za sambusa. Hakikisha tu unga siyo mlaini sana ukanatanata wakati wa kukunja sambusa

Ukaangaji wa sambusa hizi no tofauti na za kawaida. Sambusa hizi hukaangwa mara mbili. Mara ya kwanza mpaka zinapoanza tu kuwa za kahawia, unazitoa kwenye mafuta zipoe kidogo kisha unakaanga mara ya pili mpaka ziwe za kahawia vizuri kabisa. Kukaanga mara mbili inasaidia ziive vizuri na kukauka vizuri kwa nje

Moto wa kukaangia unafaa uwe wa juu kiasi, siyo mkali sana kubabua sambusa au usiwe wa chini sana kufanya zikanyonya mafuta

Kuhifadhi kwa matumizi ya baadaye ni rahisi sana kwa sambusa hizi. Unaweza kukaanga mara ya kwanza siku moja kabla ya kuliwa, unakaanga mara ya pili wakati tu wa kuweka mezani. Unatakiwa tu kuzihifadhi vizuri kwenye friji. Kama sambusa nyingine, sambusa hizi pia baada ya kukaangwa mara ya kwanza zinaweza kuhifadhiwa kwenye freezer kwa wiki kadhaa, unaziyeyusha na kukaanga tu zikihitajika
DSC00238

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji ya manda za sambusa

Vikombe 3 unga wa ngano
1/2 kikombe siagi iliyoyeyushwa
Kikombe 1 maji
Kijiko 1 cha chai mbegu za jira
Kijiko 1 cha chai chumvi

Mahitaji ya nyama

C0110T01
1/2 kilo nyama ya kusaga
Kijiko 1 cha chakula kitunguu saumu na tangawizi
Vitunguu maji 3 vya wastani
Pilipili hoho 1/2 mara 3, rangi tofauti
Chumvi kama itakavyohitajika
Pilipili manga kama itakavyohitajika
Majani ya koriander kama yatakavyohitajika

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1; kukanda unga

Changanya unga wa ngano, chumvi na mbegu za jira kwenye bakuli kubwa. Ongeza siagi iliyoyeyushwa. Changanya vizuri kwa mkono mpaka mchanganyiko uwe kama chenga chenga

Ongeza 3/4 (robo tatu) kikombe cha maji uanze kukanda, endelea kuongeza maji kidogo kidogo yakihitajika mpaka unga ushikane vizuri. Kanda hadi ulainike kabisa. Unga utakuwa mgumu kiasi ukilinganisha na wa chapati. Ikitokea unga ukawa mlaini sana na unanata, ongeza unga kidogokidogo mpaka ushike vizuri

Funika bakuli, acha unga utulie kwa dakika kama 30

Hatua ya 2; andaa nyama

Wakati unga unatulia, anza kutengeneza nyama ya kujaza kwenye sambusa. Katakata kitunguu na hoho vipande vya mraba vidogovidogo sana. Twanga kitunguu saumu na tangawizi kama hutatumia paste iliyokwishatengenezwa; katakata majani ya giligilani vipande vidogovidogo sana. Weka pembeni

Kwenye kikaangio katika moto wa juu kiasi weka nyama, kitunguu maji, kitunguu saumu na tangawizi, chumvi na pilipili manga. Changanya vizuri

Tumia mwiko kuiachanisha nyama wakati inaendelea kuiva ili isishinane. Pika mpaka nyama iive vizuri, huku ukigeuza geuza, kama dakika 15. Ikiiva ipua jikoni, acha ipoe kabisa

C0121T01

Ikishapoa kabisa, ongeza pilipili hoho na majani ya coriander. Changanya vizuri tayari kwa kukunja

Hatua ya 3; kukunja sambusa

Kanda unga tena, ugawanye kweye madonge ya mduara 8. Kama muda unaruhusu weka madonge ya unga kwenye sehemu iliyonyunyiziwa unga, acha yapumzike kwa dakika chache kabla ya kusukuma

Sukuma kila donge utengeneze umbo la mduara kama la chapati; nyembamba kuliko chapati lakini nene kuliko manda za sambusa za kawaida. Kata katitaki upate vipande viwili vilivyolingana

Kunja upande mmoja wa unga hadi katikati. Paka maji kwa kidole upande wa juu ulipokunja kwa juu. Kunja na upande mwingine ufunike upande uliokunja mwanzoni ambao umepakwa maji kwa juu. Tengeneza kama umbo la koni. Hakikisha umefunga vizuri hakuna tobo kwa chini

Jaza nyama kwa ndani. Usijaze sana, ukijaza sana itakuwa ngumu kufunga sambusa vizuri. Hakikisha unabakiza nafasi ya kufungia. Paka maji kona za sambusa kwa kidole. Sukuma upande wa manda uliobebana kwa ndani kufunika nyama. Funga upande wa juu ambao una ubichiubichi wa maji. Hakikisha sambusa imefunga kabisa. Angalia video kwa maelekezo zaidi

Rudia na sambusa nyingine hadi umalize

Hatua ya 3; kukaanga sambusa

Kwenye kikaangio katika moto wa wastani, chemsha mafuta ya kukaangia. Ongeza sambusa chache chache, hakikisha huzijazi sana zikasongamana. Kaanga kwa dakika chache, zitoe kwenye mafuta zikianza kupata rangi ya kahawia

Toa kwenye mafuta, weka kwenye sahani yenye tissues kwa juu mafuta yachuje. Rudia kukaanga zilizobakia

Ukimaliza kukaanga zote, rudia kuzikaanga mara ya pili. Wakati huu mpaka ziwe na rangi nzuri ya kahawia na zikauke vizuri kwa juu. Kumbuka unaweza kuziweka sambusa kwenye friji kabla ya kukaanga mara ya pili. Kaanga mara ya pili ukiwa tayari kwa ajili ya kuliwa ili zitengwe za moto

Enjoy za moto na kinywaji cha baridi au cha moto

DSC00243

Comments

Join discussion.