Skonzi ni mkate mtamu sana unaopendwa na wengi na pia ni rahisi kutengeneza. Unaweza kuliwa kama kitafunwa cha chai asubuhi, au mlo kamili wa mchana na jioni ukisindikizwa na supu au mchuzi

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Saa 1 Dakika 45 Idadi ya walaji 6 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Vipimo ni muhimu sana katika kuoka. Kama unataka matokeo mazuri katika uokaji, fuatilia vipimo kama vilivyo, kamwe usikadirie chochote. Tumia vikombe na vijiko maalum kwa kupimia ili kupata matokea mazuri zaidi

Maziwa ni muhimu kakita uokaji wa skonzi. Yanasaidia ziwe laini zaidi na zichambuke vizuri. Maziwa pia haswa ya full cream yanaongeza radha nzuri kwenye skonzi

Maji ya uvuguvugu ni muhimu katika uumuaji wa unga. Hakikisha maji siyo ya moto sana wala ya baridi, yawe na uvuguvugu

Siagi ni kiungo kingine kinachochangia kwa kiasi kikubwa katika kulainisha na kuongeza radha kwenye mapishi ya skonzi. Hakikisha umeitoa siagi kwenye friji lisaa limoja kabla ya kutumia ili iwe imelainika wakati wa kutumia

Kuoka hakikisha umewasha oven moto wa juu na chini na oven imepata joto kabla ya kuweka kwenye oven. Hakikisha pia oven hujawasha moto mkali sana ili skonzi zisibabuke

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

Pakiti 1 ya hamira
1/4 kikombe maji ya uvuguvugu
Vijiko 2 vya chakula sukari
Vikombe 2 unga wa ngano
1/2 kijiko cha chai chumvi
1/2 kikombe maziwa
Vijiko 2 vya chakula siagi; na ya ziada ya kupaka juu

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Changanya maji ya uvuguvugu, hamira, chumvi na sukari kwenye bakuli kubwa. Funika na kitambaa acha mchanganyiko uumuke kwa dakika kama 5

Hatua ya 2

Ukiumuka ongeza maziwa, kikombe 1 cha unga wa ngano pamoja na vijiko 2 vya chakula vya siagi iliyolainika au kuyeyuka. Anza kukanda taratibu

Hatua ya 3

Ongeza kikombe kingine cha unga wa ngano kidogokidogo huku unakanda mpaka unga ushikane. Kama unga utakuwa unanata sana, ongeza unga wa ziada kidogokidogo mpaka ushikane kabisa. Usikande kwa muda mrefu, ukikanda sana skonzi zitakuwa siyo laini sana

Hatua ya 4

Ukimaliza kukanda, funika tena bakuli na kitambaa kwa dakika kama 30.

Hatua ya 5

Paka mafuta chombo cha kuokea. Kanda unga tena kisha ugawanye kwenye madonge 9 mpaka 12. Mimi ninapenda kubwa kwa hiyo niliweka mara 9. Funika tena na kitambaa, acha unga uumuke kwa dakika kama 30

Hatua ya 6

Unga ukikaribia kuumuka, washa oven joto la 175 ili iwe imepata joto wakati unaweka skonzi kwenye oven. Funua unga kisha upake siagi kwa juu. Oka kwa dakika kama 20 mpaka 25; au mpaka skonzi ziive vizuri

Hatua ya 7

Zikiiva, toa kwenye oven kisha uzipake tena siagi wakati bado za moto. Pakua za moto

Comments

Join discussion.