Toast zinaweza kutengenezwa kwa viungo vingi tofauti kupata radha tofauti. Ni chakula unachoweza kula wakati wowote; asubuhi, mchana au jioni. Toast ni nzuri sana kiafya haswa ukitumia mkate wa brown na kuongeza viungo vyenye virutubisho kwa juu kama nyama ya kuku, mayai, samaki, mbogamboga, matunda na kadhalika. Leo tunatengeneza toast rahisi sana ya parachichi na minofu ya nyama ya kuku wa kuoka
Yaliyomo kwenye ukurasa huu:
Dakika 20 | Idadi ya walaji 1 | Rahisi |
Mambo ya kuzingatia
Mkate mzuri wa kutengenezea toast ni wa brown kama utataka toast yako iwe nzuri kiafya. Unaweza kutumia mkate wa aina yoyote unaopatikana ulipo na unaopenda wewe
Olive oil ni nzuri zaidi katika ukaangaji wa mkate. Unaweza pia kutumia siagi au mafuta mengine ya kupikia ikitokea hauna olive oil
Parachichi kwa kawaida ni kiungo kizuri sana kwenye toast. Parachichi linaongeza radha nzuri na pia lina virutubisho vya kutosha
Viungo tofauti mbali na limao, chumvi na pilipili manga vinaweza kuongezwa kwenye toast kutokana na matakwa wa mpishi na walaji
Nyama tofauti, mayai, samaki, mbogamboga na matunda yanaweza kutumika katika utengenezaji wa toast. Unaweza kubadilisha kulingana na viungo ulivyonavyo
Baslamic glaze siyo lazina kutumia, unaweza kutumia glaze nyingine tofauti au usiweke chochote
Video
Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube
Mahitaji
Parachichi 1
Slesi moja ya sour dough, au 2 za mkate wa kawaida
Minofu ya kuku au nyama kiasi chako
Maji ya limao kama yatakavyohitajika
Chumvi kama itakavyohitajika
Pilipili manga kama itakavyohitajika
Olive oil kiasi ya kukaangia
Baslamic glaze
Maelekezo hatua kwa hatua
Hatua ya 1
Anza kwa kuandaa parachichi. Ondoa maganda na mbegu kwenye parachichi, weka kwenye bakuli kisha ulipondeponde mpaka lilainike. Unaweza pia kuacha na mabongemabonge kiasi ukipenda. Ongeza maji ya limao, chumvi na pilipili manga kwenye parachichi kwa kukadiria, kicha changanya vizuri
Hatua ya 2
Katakata minofu ya kuku vipande virefuvirefu, au kata utakavyopenda kulingana na muonekano wa toast ulionao kichwani
Hatua ya 3
Chemsha kikaango katika moto wa juu kiasi, kisha ongeza mafuta kiasi. Weka mkate kisha upakaze mafuta pande zote. Pika mkate kwenye kila upande mpaka ukauke kiasi na uwe na rangi ya kahawia kiasi
Hatua ya 4
Hamishia mkate kwenye sahani. Ongeza mchanganyiko wa parachichi juu ya mkate kisha sambaza parachichi lienee kwenye mkate mzima. Ongeza minofu ya kuku kwa juu kwa kuisambaza kila mahali. Nyunyizia glaze ya baslamic au chochote utakachopenda kwa juu
Hatua ya 5
Enjoy na kinywaji cha moto au baridi sana
Comments
Join discussion.