Wali wa kukaanga ni njia mojawapo wa kubadilisha kiporo cha wali na kukifanya chakula fresh kitamu na chenye virutubisho vingi. Viungo vya muhimu katika wali huu kutokana na waanzlishi wake ni kitunguu saumu, mayai na sosi ya soya. Unaweza kuongeza viungo vyovyote utakavyopenda wewe kama mbogamboga, nyama, sausages, samaki na kadhalika. Kwa leo tumetumia sausages, karoti na brokoli kukamilisha pishi letu
Yaliyomo kwenye ukurasa huu:
Dakika 30 | Idadi ya walaji 4-6 | Rahisi |
Mambo ya kuzingatia
Kiporo cha wali wa baridi kinapendeza zaidi kwenye pishi hili kuliko wali fresh. Ukitumia kiporo, wali utatoka vizuri zaidi. Endapo unatumia wali fresh, unaweza kusambaza kwenye chombo cha kuokea ukaweka kwenye freezer kwa dakika 10 mpaka 15 kabla ya kupika
Sosi ya soya ni moja ya viungo muhimu sana kwenye kupika wali wa kukaanga. Sosi ya soya inaongeza radha na rangi nzuri kwenye wali
Mafuta ya ufuta yanaongeza radha nzuri sana kwenye wali huu, ila kuwa muangalifu ukizidisha kidogo sana yanaharibu radha nzima. Mafuta ya ufuta yana harufu nzito kwa hiyo tumia kiasi kama maelekezo kwenye vipimo
Viungo tofauti kama nanasi, zabibu kavu, mbogamboga za aina tofauti, nyama za aina tofauti, samaki wa aina tofauti na kadhalika vinaweza kuongezwa kwenye wali
Mapishi ya wali wa kukaanga ni rahisi na yanaenda haraka sana. Hakikisha umeandaa viungo vyote kabla ya kuanza kupika. Ukichelewa kidogo viungo vinaweza kupitiliza kuiva au hata kuungua na kuharibu ubora na radha ya chakula
Kukaanga mayai unaweza kukaanga mayai pembeni ukayakatakata kisha ukachanganya mwishoni kwenye wali au kuyakoroga wakati wa kukaanga kama nilivyofanya
Video
Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube
Mahitaji
Vikombe 4 vya chakula wali uliopikwa
200g sausages utakazopenda
Karoti 2 za wastani, menya na katakata vipande vidogovidogo vya mraba
Kikombe 1 brokoli, katakata kama vimaua
Mayai 3, yapige
Vitunguu vya majani 4, gawanya vyeupe na kijani
1/3 kikombe mahindi ya kuchemsha ya ya kopo
Vijiko 3 vya chakula mafuta ya kupikia
Pilipili manga (nyeupe) kwa kuonja
Kijiko 1 cha chai kitunguu saumu na tangawizi
Vijiko 4 vya chakula sosi ya soya nyepesi (light)
Kijiko 1 cha chakula mafuta ya ufuta
Maelekezo hatua kwa hatua
Hatua ya 1
Andaa viungo vyote weka pembeni karibu na jiko ili usichelewe katika kuongeza viungo. Katakata sausages na karoti vipande vidogovidogo vya mraba. Gawanya vitunguu vya majani mara mbili, sehemu nyeupe ya chini peke yake na majani ya juu peke yake. Katakata na kuweka pembeni. Piga na mayai, weka pembeni
Hatua ya 2
Kwenye kikaango katika moto wa wastani, chemsha mafuta. Ongeza vitunguu sehemu nyeupe ya chini pamoja na paste ya kitunguu saumu na tangawizi. Kaanga mpaka harufu ya ubichi iishe na vilainike, ila visibadilike rangi
Hatua ya 3
Ongeza karoti na brokoli, endelea kukaanga mpaka zikaribie kuiva, ukiweka uma uingie mpaka ndani, ila zisilainike sana. Unaweza kuongeza maji kidogo sana ili mboga zisibadilike rangi na ziive vizuri
Hatua ya 4
Ongeza sausages na mahindi. Pika kwa dakika kama 2 nyingine au mpaka uone zimechanganyikana vizuri na sausages zimepata moto wa kutosha
Hatua ya 5
Tumia mwiko kuhamishia viungo vyote upande mmoja wa kikaango, kisha ongeza mafuta kiasi upande ulio wazi. Piga mayai, weka kwenye upande wenye mafuta. Yakoroge haraka sana yasipate mabonge kisha changanya kila kitu pamoja kwa haraka
Hatua ya 6
Ongeza wali na sosi ya soya. Changanya mpaka wali upate tu joto, usipike muda mrefu viungo vikaiva sana. Ongeza mafuta ya ufuta na vitunguu vya majani. Changanya na ipua haraka vitunguu vya majani visiive sana
Hatua ya 7
Pakua cha moto na enjoy na chochote utakachopenda kama chachandu, matunda, juice fresh na kadhalika
Comments
Join discussion.