Wali wa kukaanga ni njia mojawapo wa kubadilisha kiporo cha wali na kukifanya chakula fresh kitamu na chenye virutubisho vingi. Viungo vya muhimu katika wali huu kutokana na waanzlishi wake ni kitunguu saumu, mayai na sosi ya soya. Unaweza kuongeza viungo vyovyote utakavyopenda wewe kama mbogamboga, nyama, kamba wadogo, samaki na kadhalika. Kwa leo tumetumia kamba wadogo katika pishi letu

Yaliyomo kwenye ukurasa huu:

Dakika 30 Idadi ya walaji 4 Rahisi

Mambo ya kuzingatia

Kiporo cha wali wa baridi kinapendeza zaidi kwenye pishi hili kuliko wali fresh. Ukitumia kiporo, wali utatoka vizuri zaidi. Endapo unatumia wali fresh, unaweza kusambaza kwenye chombo cha kuokea ukaweka kwenye freezer kwa dakika 10 mpaka 15 kabla ya kupika

Sosi ya soya ni moja ya viungo muhimu sana kwenye kupika wali wa kukaanga. Sosi ya soya inaongeza radha na rangi nzuri kwenye wali

Mafuta ya ufuta yanaongeza radha nzuri sana kwenye wali huu, ila kuwa muangalifu ukizidisha kidogo sana yanaharibu radha nzima. Mafuta ya ufuta yana harufu nzito kwa hiyo tumia kiasi kama maelekezo kwenye vipimo

Viungo tofauti kama nanasi, zabibu kavu, mbogamboga za aina tofauti, nyama za aina tofauti, samaki wa aina tofauti na kadhalika vinaweza kuongezwa kwenye wali

Mapishi ya wali wa kukaanga ni rahisi na yanaenda haraka sana. Hakikisha umeandaa viungo vyote kabla ya kuanza kupika. Ukichelewa kidogo viungo vinaweza kupitiliza kuiva au hata kuungua na kuharibu ubora na radha ya chakula

Kukaanga mayai unaweza kukaanga mayai pembeni ukayakatakata kisha ukachanganya mwishoni kwenye wali au kuyakoroga wakati wa kukaanga kama nilivyofanya

Video

Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube

Mahitaji

Vijiko 4 vya chakula mafuta ya kupikia
350g kamba wadogo, menya na safisha
Chumvi na pilipili manga (nyeupe) kwa kuonja
Kitunguu maji 1 cha wastani, katakata vipande vidogovidogo
Karoti 1 kubwa, menya na katakata vipande vidogovidogo
1/2 kikombe njegere
Vijiko 2 vya chai kitunguu saumu
Mayai 2, yapige
Vikombe 3 vya chakula wali uliopikwa
Vijiko 3 vya chakula sosi ya soya nyepesi (light)
Kijiko 1 cha chakula mafuta ya ufuta
1/4 kikombe majani ya kitunguu

Maelekezo hatua kwa hatua

Hatua ya 1

Andaa viungo vyote weka pembeni karibu na jiko ili usichelewe katika kuongeza viungo

Hatua ya 2

Kwenye kikaango katika moto wa wastani, chemsha vijiko 2 vya mafuta. Ongeza kamba wadogo (shrimps). Wasambaze kwenye kikaango wasibebane, kama kikaango kidogo pika mara 2. Ongeza chumvi na pilipili manga kwa kuonja. Pika kwa dakika kama nne kwa pande zote, wasiive sana wakakauka. Hamishia kwenye sahani

Hatua ya 3

Ongeza kijiko kingine cha mafuta kwenye kikaango, kisha weka kitunguu maji, kitunguu saumu na karoti. Kaanga mpaka vilainike ila visiive sana. Ongeza njegere. Unaweza kuongeza na maji kidogo sana kusaidia njegere ziive vizuri na pia endapo viungo vitashika kwenye sufuria viachie. Endapo utatumia kikaangio cha ambacho hakishiki chini unaweza pia kuongeza maji kiasi kuwivisha tu njegere

Hatua ya 4

Tumia mwiko kuhamishia viungo vyote upande mmoja wa kikaango, kisha ongeza mafuta yaliyobakia upande ulio wazi. Piga mayai, weka kwenye upande wenye mafuta. Yakoroge haraka sana yasipate mabonge kisha changanya kila kitu pamoja kwa haraka

Hatua ya 5

Ongeza wali na kamba wadogo (shrimps) waliokaangwa awali. Changanya mpaka wali upate tu joto, usipike muda mrefu viungo vikaiva sana. Ongeza sosi ya soya na mafuta ya ufuta. Changanya vizuri, weka vitunguu vya majani. Changanya na ipua haraka vitunguu vya majani visiive sana

Hatua ya 6

Pakua cha moto na enjoy na chochote utakachopenda kama chachandu, matunda, juice fresh na kadhalika

Comments

Join discussion.