ZEGE au chispi mayai ni chakula kilichozoeleka sana kwenye jamii yetu hasa Tanzania na Kenya. Ni street food unayokutana nayo kila kona na kwa bei nzuri. Kumbukumbu yangu ya utoto ni kununuliwa chispi mayai ukiwa unaumwa unapewa na soda baridi, siku ukimaliza yote ndiyo siku umepona. Kwa kawaida chipsi mayai ni viazi vya kukaanga tu vinakaangwa na mayai. Unaweza kuongeza virutubisho kwa kuongeza mbogamboga tofauti pamoja na maziwa. hii pia huboresha radha na muonekano wake huleta hamu ya kula
Yaliyomo kwenye ukurasa huu:
Dakika 30 | Idadi ya walaji 1 | Rahisi |
Mambo ya kuzingatia
Kukaanga viazi inategemea na mazoea ya mpishi. Unaweza kutumia viazi fresh, frozen au ukachemsha viazi kwanza kabla ya kukaanga. Kumbuka tu kutokukausha sana chipsi, zinapendeza zaidi zikiwa laini siyo kavu sana
Mafuta ya kukaangia chipsi yanatakiwa yawe masafi. Mafuta machafu siyo mazuri kiafya na pia hubadilisha rangi ya chipsi kuzifanya zionekane chafu. Mwishoni ukiweka viungo vingine, uchafu wa mafuta unaharibu mvuto wa chakula chote
Maziwa ni kiungo kingine ambacho hakijazoeleka kwenye ukaangaji wa chispi mayai. Unaweza kutumia au kutokutumia maziwa. Unaweza pia kuongeza maji badala ya maziwa, maamuzi ya mpishi
Mbogamboga zinapendeza zikiwa hazijalainika sana. ukikatakata vipande vidogovidogo zitaiva vizuri kutosha bila kuua virutubisho. Unaweza ukaongeza na kupunguza au kubadilisha mbogamboga kutokana na matakwa ya walaji
Kugeuza chipsi mayai kwa mara ya kwanza inaweza kuwa changamoto itakayopelekea kuvunjika. Tumia sahani kwenye kugeuza kuhakikisha inatoka vizuri bila matatizo
Kukaanga mbogamboga unaweza kukaanga mbogamboga pembeni kwanza kabla ya kuweka kwenye mayai kama utataka ziive ziwe laini kabisa
Video
Angalia Video hapa jinsi ya kutengeneza hatua kwa hatua. Usisahau kusubscribe kwenye channel yetu ya YouTube
Mahitaji
Viazi 2-3 vikubwa
Mafuta ya kukaangia chispi
Mayai 3
Karoti 1 ndogo sana
Pilipili hoho 1/8 x 3, rangi tofauti
Vitunguu maji 1/2 kidogo
Nyanya 1/2 ndogo
Vijiko 3 vya chakula maziwa
Mafuta kiasi ya kukaangia mayai
Chumvi kwa kuonja
Pilipili manga kwa kuonja
Maelekezo hatua kwa hatua
Hatua ya 1
Anza kwa kukaanga chipsi kama utakavyopenda. Fanya kwa uamuzi wako kama ni kuchemsha kwanza viazi au kukaanga moja kwa moja
Hatua ya 2
Wakati chipsi zinaiva, andaa viungo vingine. Katakata kitunguu maji, karoti, pilipili hoho na nyanya vipande vidogovidogo sana vya mraba kadri utakavyoweza
Hatua ya 3
Pasua mayai, weka kwenye bakuli kubwa. Ongeza mbogamboga; kitunguu maji, nyanya, karoti na pilipili hoho (weka kiasi utakachopenda). Ongeza maziwa, chumvi na pilipili manga. Changanya vizuri
Hatua ya 4
Chipsi zikiiza hamishia kwenye kikaango kilichopata moto kwa ajili ya kukaanga na mayai. Ongeza na mafuta kiasi sana ili mayai yasichike chini
Hatua ya 5
Ongeza mchanganyiko wa mayai kwenye kikaango chenye chispi, sambaza vizuri chispi zote zifunikwe. Acha kila kitu kiive pamoja katika moto wa wastani. Kuwa muangalifu moto usiwe mkali sana. Pika mpaka mayai yaanze kuiva na kushikana, na chini yapate rangi ya kahawia kiasi
Hatua ya 6
Geuza kwa kutumia sahani ili chipsi mayai isimong´onyoke au kuvunjika. Pika upande wa pili kwa dakika chache mpaka mayai yaive vizuri ila yasikauke sana
Hatua ya 7
Pakua kwenye sahani, enjoy na kinywaji cha baridi sana
Comments
Join discussion.